NHC yataka sera unafuu kodi vifaa ujenzi

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 08:36 AM Oct 27 2024
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah
Picha:Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limetoa mapendekezo kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), kushawishi sera inayoleta unafuu wa kodi katika vifaa vya ujenzi na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wanunuzi, ili kuchochea Watanzania wengi kumiliki nyumba.

Wakati NHC ikitoa ombi hilo, Kamati imetoa tahadhari kwa serikali na kuitaka kuweka usimamizi wa majengo yake katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini hapa, ili yadumu kwa muda mrefu.

Mapendekezo hayo yalitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua miradi nane ya majengo ya wizara yanayojengwa shirika hilo, kwa gharama za Sh. bilioni 186.8 katika mji huo na kutarajiwa kukamilika Januari 31, mwakani.

Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Abdallah alisema shirika linatambua serikali ilishaanza jitihada za kuondoa VAT katika mauzo ya nyumba zilizo chini ya Sh.  milioni 50, lakini wanaona ili sekta ya nyumba iwe na ustawi mkubwa, kodi hiyo iondolewe kwa wanunuzi wote.

“Wanunuzi wa nyumba za NHC ambao ni mmoja mmoja hawawezi kurejesha VAT kwa sababu hawafanyi biashara, mwaka jana serikali ilifanya uamuzi mzuri kwa nyumba zote ambazo thamani yake haizidi Sh. milioni 50 zinaondolewa VAT na hilo linafanyika.

 â€śLakini sisi tuna kiu ya kuona walau wanunuzi wote wa nyumba waondolewe hiyo kodi, kwa kuwa shirika litakuwa limelipa kodi zote za serikali zinazohitajika, ili kuwafanya Watanzania wamudu kulipa fedha zinazohitajika katika ununuzi wa nyumba, ”alisema.

Alisema kwa sasa serikali imefanya vizuri kwenye sekta ya kilimo na mikopo yao ni kwa riba ndogo na kupendekeza kamati iishauri serikali kuangalia namna ya kuwawezesha Watanzania wanaochukua mikopo ya nyumba, wapate kwa riba ndogo.

“Haya yote tumewasilisha kwa kamati wameyabeba kwa kuwa mengine ni ya kisera, ili kuangalia ni kwa kiwango gani riba zitapungua ina Watanzania waondokane na upangaji waingie katika umiliki wa nyumba,” alisema.

Alisema mahitaji ya nyumba kwa mwaka ni 200,000, hivyo ni muhimu kuwa na mkakati wa kupunguza uhitaji huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma, alisema kamati imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa majengo hayo ambayo NHC ni mkandarasi na kusisitiza ikamilike kwa wakati uliopangwa.

“Tumeona majengo mengi hatua za ujenzi zipo zaidi ya asilimia 80 na wapo ndani ya mkataba waliowekewa, tunaamini watakamilisha ndani ya muda uliopangwa. 

“Miradi hii itaipa nguvu NHC ijiendeshe kwa tija zaidi, ninaipongeza bodi kwa usimamizi mzuri wa shirika hili ambalo tunaona limefanya mageuzi makubwa yenye tija,”alisema.

Kuhusu utunzaji wa majengo, Mwenyekiti huyo alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa majengo katika mji huo na yapo mbioni kukamilika, hivyo ni vyema kuangalia namna ya kuyatunza vizuri.

“Huu mji kwa sasa unang’aa na serikali imetumia mabilioni kuujenga, baada ya muda fulani utakutana na uchakavu majengo yatakuwa hayang’ai kama yanavyong’ara kwa sasa.

“Majengo mengi ya serikali yamekuwa yakijengwa na kukamilika vizuri, baada ya muda ukienda unakuta miundombinu yote ya maji, majitaka na mwonekano wa jengo inakuwa changamoto,” alisema.