Wachimbaji madini wampa tuzo Rais Samia

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 12:10 PM Oct 20 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Mitambo ya Uchorongaji kwa ajili ya Wachimbaji wadogo na Mitambo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwenye hafla iliyofanyika Dodoma tarehe 21 Oktoba, 2023.
Picha:Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Mitambo ya Uchorongaji kwa ajili ya Wachimbaji wadogo na Mitambo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwenye hafla iliyofanyika Dodoma tarehe 21 Oktoba, 2023.

WACHIMBAJI wa madini katika mikoa ya Songwe na Mbeya, kwa kushirikiana na kampuni ya MC Edwin Luvanda Branding and Entateiment, wamemtunuku tuzo Rais Samia Suluhu Hassan, kutambua mchango wake katika kukuza sekta ya madini nchini.

Tuzo hiyo waliikabidhi juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, wakati wa hafla ya usiku wa dhahabu iliyofanyika wilayani hapa na kuwashirikisha wachimbaji madini kutoka mikoa ya kimadini ambayo ni Mbeya, Chunya na Songwe. 

Mkurugenzi wa kampuni hiyo iliyoandaa tuzo hiyo, Edwin Luvanda, alisema wameamua kutoa tuzo hiyo kwa rais, kwani amekuwa mstari wa mbele katika kukuza sekta ya madini, hivi sasa wachimbaji wananufaika madini ukilinganisha na huko nyuma. 

Nao Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya, Njumbo Mtawa na Kaimu Mwenyekiti wa  Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Songwe, Goodluck Mungure, walisema serikali imefanya kazi kubwa kuinua sekta ya madini ambapo hivi sasa kuna soko la uhakikika la kuuza madini hapa nchini. 

"Zamani mfano sisi wachimbaji dhahabu tulikuwa tukilazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam au mkoani, kwa ajili ya kwenda kuuza madini hali ambayo ilikuwa hatari kiusalama usumbufu huo hivi sasa haupo masoko yanapatikana karibu," alisema Mtawa. 

Naye Homera alisema kwa kutambua kuwa dhahabu ni uchumi, biashara na pia ni maisha atawaelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wafike kutoa elimu kuhusu kodi mpya ya asilimia mbili wanayotozwa wachimbaji, ili wawe na uelewa mzuri.

"Alikuja Kamishna wa TRA mkoani kwetu, alifika hadi kwenye mpaka wa Kasumulu wilayani Kyela na kuahidi kushughulikia changamoto zote zinazowakabili wachimbaji," alisema.

Homera aliipongeza kampuni ya MC Edwin Luvanda Branding and Entateiment, kwa kuandaa maonesho ya vifaa vinavyotumika kwenye uchimbaji pamoja hafla ya usiku wa dhahabu na kwamba yatafanyika mjini Mbeya.

Aidha, Homera aliwataka wachimbaji wa madini wakipata pesa zinazotokana uchimbaji wazitumie, kwani hakuna atakayeishi milele hapa duniani.

"Ukipata pesa kula maisha hakuna atakayeishi hapa duniani milele," alisema Homera na kuwatangazia wachimbaji hao kuwa mkoa umeandaa festiva 2024 ya nyama choma, itakayofanyika ufukwe wa Matema, Ziwa Nyasa wilayani Kyela," alisema.