WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ametishia kufuta leseni za uchimbaji madini kutokana na baadhi ya wamiliki kuhodhi bila kutumika na kugawa kwa wengine.
Mavunde alitangaza msimamo huo katika mgodi wa Kasubuya ulioko wilayani hapa Mkoa wa Geita wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mwishoni mwa wiki iliyopita. Amesema kuwa wamiliki hao wanatakiwa kuzingatia Sheria ya Madini Sura ya 123 na Kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao kuhusiana na leseni hizo.
Mavunde, alionya leseni hizo hazipaswi kupangishwa wala kuachwa bila kuendelezwa na kuwahimiza wamiliki hao kuzingatia kanuni mpya kuingia makubaliano na wamiliki wa maduara na kusajili Ofisi ya Tume ya Madini.
“Mtu yoyote ambaye amepewa leseni anatakiwa aiendeleze. Hakuna kuhodhi eneo bila shughuli za maendeleo. Leseni zote zisizoendelezwa nataka niwahakakikishie ninakwenda kuzifuta mara moja ili wapewe wengine wenye uwezo wa kuziendeleza,” alisema.
Awali, alisema wachimbaji wadogo kwa sasa wanachangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya taifa yatokanayo na sekta ya madini. Mavunde, alisema mchango wao unaendelea kuongezeka kutokana na maboresho makubwa ya Sheria, Kisera na Kiutendaji yanayofanywa na Serikali.
Alisema tangua mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2024, kuanzia Oktoba 1, mwaka jana, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua zaidi ya tani 15 za dhahabu hadi sasa na kuiwezesha Tanzania kuingia kwenye orodha ya nchi 10 bora barani Afrika zinazomiliki hifadhi kubwa ya madini hayo.
Kuhusu kuboresha huduma za uchunguzi wa madini, Mavunde, alisema Serikali inajenga maabara tatu kubwa mikoa ya Geita, Dodoma na Chunya (Mbeya) kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wachimbaji.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika utafiti wa kina wa madini, hivyo wizara hiyo kwa sasa inajipanga kwa ununuzi wa helikopta kwa ya kubaini maeneo yenye rasilimali hiyo chini ili kusaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.
Kuhusu kupanda kwa bei na upungufu wa kemikali ya sayanaidi nchini, alisema wanatarajia kufanya kikao maalum kati ya Wizara hiyo, Tume ya Madini na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kesho kutafuta suluhisho kwa wachimbaji wadogo.
Waziri huyo, alitoa wito kwa wachimbaji wa madini nchini kudumisha amani katika maeneo yote ya uchimbaji nchini na kufanya shughuli zao kwa utulivu. “Tanzania ni nchi ya amani. Naomba tuendelee kuilinda kwa wivu mkubwa na kuheshimiana katika shughuli za uchimbaji,” aliwaasa wachimbaji hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, alimpongeza Waziri huyo kwa usimamizi imara katika sekta ya madini nchini na kuendelea kunufaisha wachimbaji wadogo.Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Nassor Amar, aliomba leseni za utafiti ambazo hazifanywi kazi zifutwe na kugawiwa kwa wachimbaji wadogo.
Mwenyekiti wa Vijana Wachimbaji Madini Taifa, Khamis Mohamed, alimshukuru Waziri huyo kwa kuendeleza programu ya MBT na kuomba maeneo yenye taarifa sahihi ya uwepo wa madini yatengwe kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED