Mac x, Youtong zaua watano Monduli

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 06:00 PM Nov 23 2025
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Justine Masejo
PICHA: MTANDAO
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Justine Masejo

WATU watano wamepoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea leo mchana, eneo la Mbuyuni, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Ajali hiyo imeyahusisha gari dogo aina ya Toyota Mac X, lenye namba za usajili T 705 DFP iliyokuwa ikitokea Arusha, kugongana na basi la abiria aina ya Youtong, lenye namba T 922 DZQ lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Arusha.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Justine Masejo, amesema ajali hiyo imetokea leo mchana majira ya saa 7:00.

Katika ajali hiyo, Kamanda Masejo amesema imesababisha pia majeuhi kwa abiria mmoja.

"Waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume watatu na wanawake wawili. Kwa upande wa majeruhi ni mwanamke ambao wote walikuwa ni abiria katika gari dogo,"amesema.

Aidha, Kamanda Masejo amesema chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa.

Majeruhi wa ajali hiyo amelazwa katika Hospitali ya Jeshi Monduli kwa ajili ya matibabu, na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Makuyuni.

Masejo ametoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto, kuchukua tahadhari na kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, wakati wote waendeshapo vyombo vya moto ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea.