Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa, ameonya watumishi wa umma dhidi ya kutumia mabavu na sheria kandamizi wanapotekeleza majukumu yao kwa wananchi. Ametoa onyo hilo leo wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Chakula na Vipodozi uliofanyika katika ofisi za halmashauri.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wajumbe nane wa kamati pamoja na wageni kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) akiwemo Mkaguzi wa Kanda ya Kusini, Inj. Manyama, na Bw. Mwinyi Mghamba, Afisa Afya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Akizungumza katika hafla hiyo, DED Chionda aliwapongeza wajumbe kwa kuteuliwa na kusisitiza kuwa uteuzi wao umezingatia uwezo na sifa walizonazo. Alisema kamati hiyo ni ya kisheria na inatarajiwa kutekeleza majukumu yake kwa umakini na weledi, huku akiitaka halmashauri kuwapatia mafunzo maalum ili kuwaongezea uwezo.
“Kamati ijikite katika kutoa elimu kwa jamii na wafanyabiashara. Naonya matumizi ya mabavu na sheria kandamizi kwa wananchi. Sisi tusiwe kikwazo kwa wananchi; narudia tena, elimu iwe kipaumbele,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa TBS Kanda ya Kusini, Inj. Manyama, amepongeza kuundwa kwa kamati hiyo na kueleza kuwa inaleta nguvu mpya katika usimamizi wa ubora wa bidhaa. Alisisitiza kuwa jukumu la wakaguzi si kukusanya kodi bali kutoa elimu kwa watoa huduma ili kuhakikisha bidhaa zinafuata viwango.
Aidha, Bw. Mwinyi Mghamba, Afisa Afya Mkoa, aliunga mkono uanzishwaji wa kamati hiyo akisema itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri kupitia usimamizi sahihi wa shughuli za chakula na vipodozi.
Awali, Bi Zena Bingwe, Mratibu wa Usalama wa Chakula na Vipodozi, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kitengo hicho. Aliyataja baadhi ya majukumu kuwa ni kuimarisha mtandao wa watoa huduma, kupokea maombi ya utoaji wa huduma za chakula, kusajili na kutoa vibali, pamoja na ukaguzi na uchukuaji wa sampuli za vyakula kwa kushirikiana na TBS.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED