Serikali imesema itafanya mazungumzo na wafadhili ambao wameonyesha nia ya kujitoa kufadhili miradi mbalimbali nchini kufuatia matukio yaliyotokea Oktoba 29,2025 wakati wa uchaguzi mkuu.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Amesema baadhi ya wafadhili wameonyesha wasiwasi kutokana na yaliyotokea wakati wa uchaguzi , lakini akasisitiza kuwa mazungumzo yanaendelea wanatumaini watafikia makubaliano. “Ni kweli kutakuwa na mtikisiko katika maeneo fulani kiuchumi, Serikali inatambua hali hiyo na tupo tayari kuhakikisha mambo hayakwami,” amesema.
Ameeleza kuwa licha ya baadhi ya wadau kutangaza kusitisha ufadhili, miradi mingi ya maendeleo nchini inaendelea kutekelezwa kwa fedha za ndani. Hivyo, juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo hazitasimama.
Ameongeza kuwa Serikali imejiandaa kukabiliana na athari zozote zitakazojitokeza ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma muhimu bila usumbufu. “Serikali inawajali wananchi wake ipo makini na itahakikisha inasimamia maslahi ya Taifa na kuendeleza miradi yote muhimu,” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED