Shinyanga Polisi Jamii Marathon yasisitiza kulinda amani ya nchi

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 04:06 PM Nov 30 2025
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Patrobas Katambi akiongoza Mbio za Shinyanga Polisi Jamii Marathon.
PICHA: MARCO MADUHU
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Patrobas Katambi akiongoza Mbio za Shinyanga Polisi Jamii Marathon.

MBIO za Shinyanga Polisi Jamii Marathon zimefanyika mjini Shinyanga, zikishirikisha wakimbiaji kutoka Shinyanga, Tabora Mbongwe, Kahama na Misungwi, huku ukitolewa ujumbe wa kuimarisha amani na usalama wa nchi.

Mbio hizo zimefanyika leo Novemba 30, 2025 katika Viwanja vya Sabasaba, zikihusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21 ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Patrobas Katambi.

Katambi akizungumza na washiriki wa mbio hizo, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuwa karibu na jamii na hata kuandaa Marathon, kwa ajili ya kuwaweka karibu na kujenga mahusiano mazuri.

Amesema michezo ni Afya,kuwaunganisha watu kuwa wamoja, undugu, ujamaa na kuishi kwa upendo na furaha, huku akiwaomba Watanzania kuendelea kuilinda amani ya nchi yetu kama iliyoachwa na waasisi wa taifa hili na wasikubali kuichezea kwa maslahi ya watu wachache.

“Mlichokifanya Jeshi la Polisi kupitia Mbio hizi za Marathon ni kupandikiza Mbegu ya Uzalendo kwa wananchi, ambao tunawaomba sasa waendelee kudumisha amani ya nchi yetu ili tuishi kwa upendo na utulivu,”amesema Katambi.

Aidha, amesema serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono shughuli za michezo, na kuwataka wananchi waendelee kumuunga mkono Rais katika juhudi zake za maendeleo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, ambaye pia ni mlezi wa Polisi Jamii Fitness Center, amesema marathon hiyo imelenga kuimarisha undugu na kuwakutanisha wananchi na Jeshi la Polisi ili kuongeza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama.

Amesema Jeshi la Polisi linapokuwa karibu na wananchi wanaishi vizuri hakuna uharifu pamoja na kuendelea kudumisha amani ya nchi, na ndiyo maana mkoa wa Shinyanga upo shwari amani inaendelea kutawala na kila mtu anafanya shughuli zake.

katika marathon hiyo washindi walipatiwa zawadi ya fedha taslimu, pamoja na kutunuku vyeti kwa viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamefanikisha jambo hilo. Kauli Mbiu ya Marathon hiyo inasema”Kimbia kwa Afya Imarisha usalama wa Raia na Mali zao”.