Tukio moto Mlima Hanang’ waibua kumbukizi za maafa ya maporomoko

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 09:08 AM Dec 07 2025
 Tukio moto Mlima Hanang’ waibua kumbukizi za maafa ya maporomoko
Picha:ITV
Tukio moto Mlima Hanang’ waibua kumbukizi za maafa ya maporomoko

Ni maajabu ya Musa. "Ndivyo inavyoweza kuelezwa, baada ya moto mkubwa, ambao haujajulikana chanzo chake kuzuka katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mlima Hanang' ulioko mkoani Manyara."

Moto huo, ulioanza Disemba 3 mwaka huu na kuharibu sehemu kubwa ya hifadhi hiyo ya mazingira ya Mlima Hanang, unafanana tarehe na mwezi uliotokea maafa ya Hanang' yaliyosababisha vifo vya watu 89 na kujeruhi wengine 116, Desemba 3 mwaka 2023.

Ofisa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Abubakary Mpapa, amesema moto huo uloanza Desemba 3 mwaka huu, umeharibu zaidi ya hekta 170. 

Huku, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Emmanuel Kiabo, akisema jitihada za kuzima zinaendelea, ili kuzuia kusambaa kwa moto kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu jirani na mlima.

Inaelezwa kuwa, chanzo cha moto huo huenda kimesababishwa na shughuli za kibinadamu, hasa kurina asali kwa kutumia moto.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ametoa wito kwa wananchi kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu mlima, ikiwemo kurina asali kwa kutumia moto na uvutaji wa sigara.

Kwa upande wake, Mbunge wa Hanang (CCM), Asia Halmga, amewahimiza wananchi kusaidia katika jitihada za kuzima moto unaosambaa haraka.