WANANCHI 866 wamenufaika na mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ambayo yanatolewa na Chuo cha ufundi stadi(VETA) Gorowa kilichopo wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Akitoa taarifa ya chuo hicho jana katika mahafali ya nne Mkuu wa Chuo, Joshua Matagane alisema wananchi 680 waliopata mafunzo ya muda mfupi wanaume ni 511 na wanawake 169. Aidha alisema toka Chuo kianze Julai 2020 chuo hicho kimetoa mafunzo ya muda mrefu kwa vijana 186 wa kiume 117 na wa kike 69 huku akisema mwaka huu wanahitimu vijana 38 wa kiume 21 na wa kike 17.
Mkuu huyo alisema chuo kinafundisha umeme wa majumbani, ufundi bomba na ushonaji wa nguo na ubunifu wa mitindo huku akisema mwaka ujao wataongeza fani zingine. Naye mkuu wa wilaya ya Babati Emmanuela Kaganda alisema ujuzi walioupata utawasaidia na kuajiri watu wengine.
Kaganda alisema serikali itaendelea kuimarisha sera na kutoa mafunzo ya ufundi stadi maeneo ya vijijini. Kwa upande wake msoma risala ambaye ni mhitimu Saumu Ally aliiomba serikali kuwajengea maktaba na kuongeza fani nyingine.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED