DUCE yaendelea kutoa wahitimu wenye umahiri sekta elimu

By Pilly Kigome , Nipashe Jumapili
Published at 07:37 AM Dec 01 2025
Wahitimu mahafali ya 18 DUCE
Picha: Mpigapicha Wetu
Wahitimu mahafali ya 18 DUCE

CHUO Kishiriki cha Elimu Cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dar es Salaam kimewatunuku jumla ya wahitimu 1,823 wa Stashahada, Shahada za Awali na Shahada za Uzamili za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani mbalimbali katika Mahafali ya 18 yaliyofanyika chuoni hapo.

Kati ya hao wahitimu wa kike ni 1,008 sawa na asilimia 55.3 ya wahitimu wote na wa kiume ni 815 sawa na asilimia 44.7. 

Hayo yamesemwa Novemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam na Rasi wa Chuo Kishiriki Cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof. Stephen Maluka katika Mahafali ya 18 ya chuo hicho.

Prof. Maluka amesema kukamilika kwa mahafali hayo ya 18 kinafanya chuo hicho kufikisha jumla ya wahitimu 23,547 waliobobea katika fani mbalimbali tangu kuanzishwa kwake na kwenda kuwa mchango mkubwa katika sekta ya elimu na katika kuzisaidia jamii zetu na serikali kwa jumla kufikia malengo yake.

Amesema katika kutimiza wajibu chuo kinatoa wahitimu bora wanaokubalika katika soko la ajira na kuchangia maendeleo ya taifa.

Katika utekelezaji wa suala hilo mahafali yameshuhudia kutoa wanafunzi wanne  bora na kati ya waliyohitimu  wamevunja rekodi kwa kupata ufaulu wa juu wa GPA ya 4.7 kila mmoja katika digirii ya awali ya elimu, sayansi, insia na sayansi ya jamii.

“Wahitimu wetu wa leo wamepikwa kwa maarifa ya darasani na katika masuala ya kijamii. Hivyo ni matarajio yetu kuwa watakuwa watumishi wenye maadili na wanajumuiya wanaokubalika kwenye jamii, wazalendo na waadilifu”. amefafanua.

Aidha amefafanua kuwa chuo kinaboresha utendaji kazi wake na kupunguza changamoto ya matumizi ya wahadhiri wa muda ambao hukigharimu chuo kiasi kikubwa cha fedha. 

Kwa Mwaka 2024/2025, wafanyakazi wapatao 38 wa Chuo walirejea kutoka masomoni, ndani na nje ya nchi, na hivyo kupunguza idadi ya wahadhiri wa muda na kuokoa fedha ambazo zimeelekezwa katika matumizi mengine ya Chuo.

Kutokana na uwekezaji huo chuo kina jumla ya wanataaluma wenye digirii za udaktari wa falsafa 142, ambapo wanawake ni 52 (37%) na wanaume ni 90 (63%). Kati ya  hao Profesa ni mmoja, Maprofesa Washiriki ni saba, Wahadhiri Waandamizi 36 na Wahadhiri ni 98.

DUCE ina shule za awali za mazoezi, msingi na Sekondari katika mitihani ya Kitaifa iliyofanyika mwaka huu shule imefanikiwa kupata wastani wa ufaulu wa Daraja A katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi na Shule ya awali imeendelea kuwa kitovu cha malezi bora ya kitaaluma.

Aidha amefafanua chuo kilipata Sh. bilioni 19 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu na majengo na kujenga majengo mawili ya ghorofa na miundombinu mingine mipya ambapo ukarabati umekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa majengo mapya mawili unaendelea vizuri na umefikia wastani wa asilimia 70.

Kwa mwaka 2024/2025 chuo kimekuwa na miradi 16 ya tafiti  mojawapo ni wanataaluma wameweza kuandika machapisho zaidi ya mia moja.

Wakati huohuo aliwakumbusha wahitimu kuwa ujana na siha njema ni fahari ya taifa lolote kwakuwa vijana ni nguzo muhimu katika ujenzi wa uchumi imara katika jamii za nchi mbalimbali.

“Katika mwaka ujao wa masomo 2026/2027 chuo chetu kinatarajia kudahili wanafunzi katika programu mpya ya Shahada ya Uzamivu katika Lugha za Kiafrika (yaani PhD in African Languages) niwaombe na ninawakaribisha sana”amefafanua.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi DUCE, Prof. Willium Anangisye, amesema katika uhai wake wa miaka 20 toka kuanzishwa kwake hicho Julai 22,2005, chuo kimeendelea kupata mafanikio makubwa ikiwemo serikali kuleta majengo mapya chini ya Mradi wa HEET.

Amesema kukamilika kwa ujenzi huo utaboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na miundombinu ya kujifunzia.

Aidha, chuo kimeendelea kufanya vizuri katika nyanja za utafiti, ubadilishanaji maarifa, menejimenti ya rasilimali watu, na utoaji wa huduma za jamii.

Pia serikali imeendelea kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu katika chuo hicho.

Mwenyekiti wa Baraza DUCE, Balozi Mwanaidi Sinare amesema mafanikio ya chuo hicho yanatokana na kujitoa, kujituma kwa weledi kuhakikisha kuwa chuo hicho kinafanya vyema katika nyanja zote.

“Tunaishukuru sana serikali, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutupatia fedha za kutekeleza miradi yetu mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha miundombinu ya chuo na kuatuafanya tuendele kuzalisha wahitimu bora kutoka chuoni hapa,” amesema.