BoT yaonya matumizi ya fedha za kigeni ununuzi bidhaa nchini

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 12:31 PM Nov 23 2024
Fedha  za kigeni.
Picha:Mtandao
Fedha za kigeni.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeonya kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini kwenye mauzo ya bidhaa au huduma kuwa ni kinyume cha Sheria ya Benki Kuu Kifungu cha 26.

Onyo hilo limetolewa wakati ikishuhudiwa baadhi ya wauza bidhaa na watoa huduma kutaka kulipwa kwa fedha za kigeni hasa dola hali inayoleta usumbufu kwa wateja.

Taarifa iliyotolewa juzi na benki hiyo kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram imeeleza kuwa imebaini uwapo wa baadhi ya bidhaa na huduma kuendelea kufanyika kwa kutumia fedha za kigeni,  jambo ambalo ni kinyume na sheria ya benki hiyo.

“Bidhaa na huduma hizo ni pamoja na kuuza au kupangisha nyumba, viwanja na ofisi, ada za shule, pamoja na malipo na ushauri,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa benki hiyo pale wanapolazimishwa kulipia huduma kwa kupitia fedha za kigeni ili sheria ichukue mkondo wake.

Kadhalika iliwakumbusha wananchi kuwa ni muhimu kutumia Shilingi ya Tanzania wakati bei na kufanya malipo ya bidhaa na huduma ili kuendelea kuimarisha uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya BoT, matumizi ya shilingi nchini yataiwezesha benki hiyo kutekeleza sera ya fedha ili kuwezesha kuwapo kwa utulivu wa bei za bidhaa na huduma nchini.

Pia ilisema kupunguza matumizi ya fedha za kigeni yasiyo ya lazima ili kuimarisha thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni.

“Matumizi ya shilingi nchini yataimarisha ustahamilivu wa sekta ya fedha na kuvutia wawekezaji hivyo kuongeza pato la nchi na kuinua uchumi kwa ujumla,” ilisema taarifa hiyo.