Majaliwa: Andaeni Mitaala kuwezesha vijana wetu kujiajiri

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 12:37 PM Nov 23 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua kitabu cha tafiti za biashara 114 zilizoandaliwa na watafiti mbalimbali wa masuala ya biashara, kwenye ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua kitabu cha tafiti za biashara 114 zilizoandaliwa na watafiti mbalimbali wa masuala ya biashara, kwenye ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amevitaka vyuo vya biashara nchini kufanya mapitio ya mitaala ili kuwajenga wasomi wenye uwezo wa kutumia elimu zao kujiajiri, badala ya kuendelea kusubiri nafasi chache za ajira serikalini.

Majaliwa alisema hayo jana jijini hapa kwenye kongamano la kitaaluma la kuwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu biashara na mazingira wezeshi kwa maendeleo jumuishi, lililoandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Vyuo vya biashara fanyeni mapitio ya mitaala yenu ili tuwe na mitaala inayojenga wasomi wetu kupenda kubuni na kufanya biashara, wasomi wetu wa sekta ya biashara zingatieni mtaala wa biashara ili kila msomi anapomaliza masomo afikirie zaidi kufanya biashara kuliko kusubiri kuajiriwa serikalini.

“Serikalini nafasi zenyewe zimejaa na wengi ni vijana wana miaka 30, kwa hiyo ili mwingine atoke hapo mpaka awe na miaka 60. Kuna miaka mingine 30 ya kusubiri hivyo wahitimu wakiendelea kusubiri ajira serikalini wataendelea kuilaumu serikali kila siku,” alisema Majaliwa.

Aidha, alisema ili kumaliza tatizo hilo, vyuo vya biashara vipitie mitaala yake na kuanza kuwajenga wasomi baada ya kuhitimu masomo yao watumie elimu yao kufanya yale waliyosoma kubuni miradi itakayowaingizia kipato.

“Nilipokwenda kufanya ziara Kilombero nilikutana na vijana wawili wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), ambao wameamua kufanya biashara ya mchele na masoko yao wanayapata kwenye shule za bweni na maeneo mengine, hivyo natamani vijana wengi wahitimu wa vyuo wawe na mawazo kama hayo ya kujiajiri badala ya kusubiri ajira za serikali,” alisema.

Vile vile, aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara, kushirikiana na taasisi za umma na binafsi, kufikiria namna ya kuongeza ujasiriamali nchini kwa rika zote.

“Nihimize wataalam wetu kwenye taasisi za elimu kufanya tafiti na mtumie matokeo ya tafiti zenu kuboresha mazingira ya biashara, ikiwemo utengenezaji wa bidhaa hii itasaidia sana kuongeza thamani ya bidhaa zetu kuingia kwenye ushindani,” alisema.

Kadhalika, Majaliwa aliiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wadau wengine, kuimarisha mifumo ya biashara kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati pamoja na vyuo vya elimu ya juu, ili ikidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia.

Mkuu wa huo cha CBE, Prof. Edda Lwoga, alisema kongamnao hilo ni la tano kufanyika tangu mwaka 2019 ambapo jumla ya matokeo ya tafiti 114 yatawasilishwa.

Alisema lengo la kungamano hilo ni kujadiliana na kubadilisha uzoefu kuhusu tafiti zilizofanyika, zenye lengo la kuangalia fursa za kibiashara zilizopo na changamoto zake ili kuzitafutia ufumbuzi.