“Serikali kujenga kituo cha afya, Ilolo Mpya” - Waziri Lukuvi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:30 AM Sep 29 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi Isimani akiteta jambo na Mhe. Fundi Mihayo (Diwani wa kata ya Ilolo Mpya) katika Mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake kwenye Kata hiyo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi Isimani akiteta jambo na Mhe. Fundi Mihayo (Diwani wa kata ya Ilolo Mpya) katika Mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake kwenye Kata hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi, Isimani amesema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imepanga kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Ilolo Mpya, wilaya ya Iringa katika Mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kutembelea Miradi ya Maendeleo na kufanya Mikutano ya hadhara katika katika vijiji vitano ambavyo ni Luganga, Magozi, Mkombilenga, Ukwega na Ilolo Mpya vilivyopo katika Jimbo la Isimani Mkoani Iringa jana.

Amesema msingi wa maendeleo ni wananchi kujituma na mtu yeyote asipotoshe kwa kudai kwamba hakuna wananchi wanaojitolea kuleta maendeleo, naomba mshirikiane na viongozi wanaohimiza wananchi katika kujiletea Miradi ya Maendeleo.

“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassani imempendeza kujenga kituo cha afya na kwa sera ya Serikali kila kata inatakiwa kuwa na kituo cha afya,” alisema Waziri Lukuvi.
Wataalam wa (TASAF) watapita kuelezea namna kila kijiji kitakavyoshiriki katika ujenzi wa majengo ili kila kijiji kishiriki kikamilifu katika kukamilisha ujenzi wa majengo ya kituo cha afya. 

“Nawapongeza wananchi kwa miradi ya maendeleo lakini kuna mambo makubwa zaidi yanakuja ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Itunundu kwenda Iringa Mjini ambayo tayari Serikali imeshatangaza tenda,  ikiwa ni sambamba na tenda ya ujenzi wa mfereji wa Magoze,” alisema 

Kwa upande wake Afisa Uwezeshaji na Ufuatiliaji wa TASAF, Salim Mshana amesema majengo yanayotarajiwa kujengwa ni majengo 7 ili kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya.

Ujenzi utahusisha jengo la wagonjwa wa nje, jengo la mama na mtoto, jengo la maabara, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo, jengo kuhifadhia maiti, na nyumba ya waganga ambayo itakuwa mbili kwa moja na njia za kutembelea za kuunganisha  majengo hayo .