TASAF wasifu Dira 2025, wajipanga

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 05:50 PM Jul 18 2025
TASAF wasifu Dira 2025, wajipanga
Picha: Mpigapicha Wetu
TASAF wasifu Dira 2025, wajipanga

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Shadrack Mziray, amesema uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 si tukio la kisiasa bali ni hatua ya kimkakati kudhihirisha dhamira ya pamoja kuelekea kwenye Tanzania yenye uchumi jumuishi na ustawi kwa wote.

Akizungumza baada ya Rais  Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi dira hiyo jijini Dodoma jana, Mziray, amesema mpango huo wa muda mrefu unakuja wakati Tanzania ipo kwenye hatua ya uchumi wa kati daraja la chini na kulenga kufikia daraja la juu ifikapo mwaka 2050 kwa kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma.

“Uchumi tunaouelekea ni uchumi jumuishi ambapo wananchi wote wanufaike. Maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuwa na maana bila ustawi wa jamii. Ndiyo maana shughuli za TASAF zinaendana moja kwa moja na malengo ya dira hii mpya,” amesema Mziray.

Amesema TASAF imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii zilizopo katika mazingira magumu kupitia miradi ya hifadhi ya jamii, ikiwa ni pamoja na utoaji wa ruzuku kwa kaya maskini, kusaidia upatikanaji wa elimu, afya, na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, hasa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi.

Amesema dira hiyo imeainisha umuhimu wa kuwaunganisha watu wa kipato cha chini na fursa rasmi za maendeleo na kuhakikisha afua za kijamii ziwafikie walengwa kwa usahihi.

“Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 26 ya Watanzania bado wanaishi kwenye umaskini wa hali ya chini. Ni muhimu kuhakikisha watu hawa wanakuwa sehemu ya mchakato wa maendeleo, mfano kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote, tunawawezesha wananchi kupata huduma bora bila mzigo wa gharama,” amesema Mziray.

Ameongeza kuwa hata katika sekta ya elimu, watoto wa kaya maskini wamewezeshwa kwenda shule, kupata vifaa vya kujifunzia, sare na mazingira bora ya elimu kupitia msaada wa TASAF.

Amesisitiza mchango wa TASAF ni mhimili muhimu kufanikisha maendeleo jumuishi na kutoa wito kwa wananchi  kuisoma, kuielewa na kuitafsiri dira hiyo kwa vitendo.

“Tusiwe watazamaji. Tutikise jamii zetu, tushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hii. Hii si ndoto ya Serikali pekee, ni ndoto ya Watanzania wote. Tuifanye kuwa halisi,” amesema.

 Mkurugenzi wa Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa TASAF, Japhet Boaz, amesema kuzinduliwa kwa dira hiyo ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kikamilifu kuelekea miaka 25 ya kupanga maendeleo jumuishi kwa makundi yote ya wananchi.

Boaz, amesema amesoma dira hiyo kwa kina na taasisi yao imejipanga kushiriki kikamilifu kusaidia kaya maskini, wazee na jamii zilizoathiriwa na majanga.

Amesema dira hiyo inaweka msingi thabiti wa kujenga taifa lenye usawa na mshikamano kwa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.

“Kwa kasi ya sasa na malengo yaliyowekwa, ninaamini mwaka 2050 Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa si kiuchumi tu, bali pia katika ustawi wa jamii,” amesema Boaz.