TIA yajenga kampasi Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 09:46 AM Dec 21 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa Willian Amos Pallangyo.
Picha:Mtandao
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa Willian Amos Pallangyo.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Taasisi ya Uhasibu nchini (TIA) Kampasi ya Zanzibar ili kutoa fursa zaidi ya wanafunzi kujiunga ndani na nje ya nchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa Willian Amos Pallangyo, aliyasema hayo baada ya kukagua awamu ya kwanza ya ujenzi huo unaendelea eneo la Makunduchi Ng'anani Mkoa wa Kusini Unguja.

Pallangyo, alisema ujenzi huo ulianza Septemba mwaka huu baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kutoa fedha hizo na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) eneo lenye ukubwa wa hekari 56.

Alisema watahakikisha fedha hizo zilizotolewa na serikali zinatumika vizuri na kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Alisema ujenzi huo unaambatana na wa kumbi za mihadhara, vyumba vya maktaba, kompyuta na mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume.

Naibu Mkuu wa Mipango, Fedha na Utawala, Dk. Issaya Hassanal, alisema ujenzi wa kampasi hiyo utakamilika mwaka 2026 na kuanza kupokea wanafunzi wa ndani na nje ya nchi kupata elimu na kutoa wataalamu waliobobea katika fani za uhasibu, ukaguzi wa hesabu na nyingine zinatolewa na taasisi hiyo.

Hassanal, alisema ujenzi huo utasaidia kutoa ajira kwa wananchi wanaoishi maeneo jirani, wakiwamo mamalishe na babalishe na kujiongezea kipato katika familia zao.

Mhandisi wa ujenzi wa mradi huo, kutoka Kampuni ya Salem Constructions, Riziki Ringo, alisema wanatarajia kukamilisha katika kipindi cha miaka miwili kwa mujibu wa mkataba na taasisi hiyo, licha ya kuwapo kwa changamoto ndogo ndogo.