Serikali kupitia Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) imepokea boti mbili mpya za utafutaji na uokoaji (SARs) ambazo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.
Boti hizo zimewasili Julai 18, 2025 katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka Uturuki, ambako zilitengenezwa na Kampuni ya Loça Mühendislik chini ya utekelezaji wa Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (MLVMCTP).
Akizungumza wakati wa mapokezi ya boti hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Vyombo vya Usafiri Majini, Mhandisi Saidi Kaheneko, amesema ujio wa boti hizo ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa maisha ya abiria na mali katika Ziwa Victoria.“Boti hizi zina uwezo wa kasi kubwa na zimetengenezwa mahsusi kwa kazi za utafutaji na uokoaji wa haraka wakati wa dharura, hivyo zitasaidia kupunguza madhara ya ajali za majini,” amesema Mhandisi Kaheneko.
Ameongeza kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuboresha usalama wa usafiri wa majini kupitia uwekezaji kwenye miundombinu, usimamizi wa vyombo vya usafiri, na utoaji wa elimu ya usalama kwa watumiaji wa usafiri wa majini.
Boti hizo zinasafirishwq hadi mkoani Mwanza ambako ndiko zitakakofanyia kazi katika Ziwa Victoria ambalo linalotumika kwa shughuli nyingi za usafiri, biashara, na uvuvi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED