Dk.Nchimbi: Vyuo vikuu wapeni wanafunzi ujuzi wa vitendo

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 04:14 PM Nov 23 2024
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha: CCM
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi ameviagiza vyuo vikuu nchini kuwapa wanafunzi ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira pamoja na kuhakikisha elimu wanayotoa inalingana na mahitaji ya soko.

Alitoa agizo hilo jana mkoani Morogoro wakati akizungumza katika Kongamano la 24 la Mkutano wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali waliowahi kusoma katika chuo hicho.

Dk. Nchimbi alisema pengo kati ya elimu na sekta ya viwanda ni lazima lizibwe, kwamba haitoshi kwa vyuo vikuu pekee kufundisha tu nadharia bali vinapaswa kujielekeza pia katika ufundishaji wa vitendo.

Kuhusu utatuzi wa ajira, Dk. Nchimbi alisema: "Ukosefu wa ajira bado ni changamoto kubwa, lakini ni jambo linaloweza kushughulikiwa kupitia fikra za ubunifu na uvumbuzi. Lazima tuangalie mbali na mifumo ya ajira ya kawaida na kuchunguza viwanda vipya, majukwaa ya kidijitali na mwelekeo wa ajira usio wa kawaida"

Dk. Nchimbi alisema katika kuleta mapinduzi katika soko la ajira ni lazima kuendelezwe fikra za ubunifu na ustahimilivu.

"Kama wahitimu wa taasisi hii mashuhuri Mzumbe)  mmepata zana zinazohitajika kwa safari hii. Ni lazima muendeleze roho ya ujasiriamali, shauku ya uvumbuzi, na dhamira ya kujifunza maishani. Njia iliyo mbele siyo ya waoga, bali ni ya wale walio na ujasiri wa kuvunja mipaka, kuondoa vizuizi, na kubadilisha tasnia" alisema.

Kuhusu ujasiriamali, Dk. Nchimbi alisema ni muda mrefu taifa limekuwa likitegemea mifumo ya ajira za kitamaduni kama njia pekee ya mafanikio.

Alisema ni wakati sasa wa kutafakari upya fikra hizo, kwamba mustakabali wa uchumi wa Tanzania hauko tu kwenye kujaza nafasi zilizopo katika kampuni zilizopo, bali uko katika kuunda fursa mpya, tasnia mpya, na biashara mpya.

"Nawahimiza kila mmoja wenu kufikiria changamoto si kama vikwazo bali kama fursa za kuunda ajira. Nguvu ya kuunda mustakabali wa kiuchumi wa taifa letu iko mikononi mwa akili bunifu na za kijasiriamali kama zenu. Mawazo yenu, dhamira yenu, na ujasiri wenu ndiyo yatakayotufanikisha, " alisema.