Madereva 42 wa mabasi ya abiria jijini Mbeya, wamefungiwa leseni zao kwa muda wa miezi mitatu baada ya kubainika kuvunja sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuendesha kwa mwendo kasi, kupita magari katika maeneo yasiyoruhusiwa na ulevi wakiwa kazini.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa, ameyasema hayo Julai 18,2025 wakati akifanya ukaguzi wa magari stendi Kuu kabla hayaanza safari alfajiri.
Amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kudhibiti ajali na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara.
“Kuanzia Januari hadi Juni 2025, madereva 42 tayari wamefungiwa leseni kwa makosa ya usalama barabarani, Jeshi la Polisi halitakuwa na muhali kwa yeyote atakayebainika kuhatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara,” amesema SSP Kilewa.
Amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kufanya doria, ukaguzi na kutoa elimu ili kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa ipasavyo na kuongeza kuwa hatua hizo zitakuwa endelevu ili kuzuia ajali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutoka Kamisheni ya Oparesheni na Mafunzo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Fraisser Kashai, wakati wa ukaguzi hio amehakiki leseni za madereva, kupima kilevi, kukagua hali ya mabasi na kutoa elimu kwa madereva na abiria kuhusu usalama barabarani.
“Kila dereva anatakiwa kuwa na nidhamu na kuheshimu sheria. Atakayekiuka atachukuliwa hatua kali bila kusita,” amesema DCP Kashai.
Ofisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Mbeya, Shaban Mdende, amesema kuwa mabasi ya abiria sasa yana vifaa maalum vya kufuatilia mwenendo (VTS), vinavyowezesha LATRA kushirikiana na Jeshi la Polisi kubaini madereva wanaokiuka sheria hata wakiwa safarini.
“Katika madereva 42 waliofungiwa leseni, 26 walibainika kupitia mfumo wa VTS ambao unaonyesha mwenendo wa mabasi barabarani, ikiwa ni pamoja na mwendo kasi na tabia nyingine hatarishi,” amesema Mdende.
Ukaguzi huo ni sehemu ya jitihada za pamoja kati ya Jeshi la Polisi na LATRA kuhakikisha usalama wa abiria na kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED