Meno ya tembo, kiboko yampeleka jela miaka 20

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 02:11 PM Jul 18 2025
Abubakari Msangi (48) akiwa chini ya ulinzi wa Askari wa Magereza katika Ma-hakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na vipande saba vya meno ya Tembo na Kiboko.
Picha: Imani Nathaniel
Abubakari Msangi (48) akiwa chini ya ulinzi wa Askari wa Magereza katika Ma-hakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na vipande saba vya meno ya Tembo na Kiboko.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemuhukumu mfanyabiashara Abubakari Msangi (48), kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na vipande saba vya meno ya tembo na saba vya meno ya kiboko.

Msangi alidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 16, 2020, eneo la Mbagala, Dar es Salaam, akishtakiwa kwa kumiliki na kukutwa na nyara za serikali bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mkuu Gwantwa Mwankuga wa mahakama hiyo, alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo vitano. Baada ya kusikiliza na kupitia sheria upande huo umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

"Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi bila kuacha shaka lolote. Mahakama inakutia hatiani, hivyo shtaka la kukutwa unamiliki nyara hizi adhabu yake kifungo cha miaka 20 gerezani," alisema Mwankuga.

Alisema kuwa shtaka la kukutwa na vipande saba vya meno ya tembo na saba vya meno ya kiboko, adhabu yake ni miaka 20 jela ambapo adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja, hivyo ni miaka 20 jela.

"Mshtakiwa ninamtia hatiani kwa mashtaka mawili kama alivyoshtakiwa, hivyo kila shtaka ninakuhukumu miaka 20 jela, lakini adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja, ni miaka 20 jela badala ya miaka 40," alisema.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Pancrasia Protas aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria, ili iwe fundisho kwake na jamii.

Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea, ni mgonjwa wa saratani ya jicho na analea mtoto yatima ambaye yuko kidato cha kwanza.