Rais Samia Suluhu Hassan ameacha alama mkoani Simiyu anapohitimisha ziara yake leo, Juni 19, 2025, kabla ya kuelekea Mwanza kuandika historia nyingine kwa kufungua rasmi Daraja la JP Magufuli, Kigongo – Busisi, ambalo ni la sita kwa urefu Barani Afrika.
Pia anahitimisha ziara hiyo mkoani humo kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulioko Nyashimo, Busega, utakaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya kupunguza au kumaliza changamoto ya huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa huo.
Ziara hiyo imeacha alama katika sekta mbalimbali, ikiwamo mifugo, kilimo, maji na jinsi mikutano yake imevutia maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza kila alikozungumza, akiwa kwenye miradi au mikutano ya hadhara tangu siku ya kwanza alipopokelewa mkoani humo, eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega, Juni 15, 2025.
Katika sekta ya mifugo, Rais Samia alizindua kampeni ya kitaifa ya mpango wa miaka mitano ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima. Kinachofanya kampeni hiyo kuwa ya kihistoria ni ukweli kuwa mara ya kwanza na mwisho Tanzania ilifanya chanjo hiyo wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Jambo jingine la kihistoria katika kampeni hiyo ni faida kubwa zitakazotokana na hatua hiyo muhimu, ambayo itasaidia kulinda afya ya mifugo (na wafugaji wenyewe), kuongeza uzalishaji na ubora, na kusaidia mazao ya mifugo ya Tanzania kupata uhakika wa soko la ndani na nje ya nchi, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye mifugo mingi barani Afrika.
Kwa umuhimu wa hatua hiyo, Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), kupitia kwa Mwenyekiti wake Ndugu Murida Mshota Marocha, walimkabidhi Rais Samia tuzo ya heshima na shukrani, wakitambua kuwa hatua hiyo itaimarisha na kuiinua zaidi sekta ya mifugo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, kwa kuchangia asilimia 6.2 ya pato la taifa na kuwa chanzo cha ajira kwa kaya milioni 4.6 nchini.
Eneo jingine ni maelekezo mahsusi aliyoyatoa kwa lengo la kulinda na kuinua kilimo cha mazao ya kibiashara mkoani humo, hususan zao la kihistoria linalobeba uchumi wa wananchi wa Simiyu, pamba, pamoja na zao lingine ambalo limeanza kulimwa kwa kasi, la mbaazi.
Mbali na maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kuhusu utoaji wa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu, ufuatiliaji wa hali ya soko na bei nzuri, usimamizi wa ushirika, mifumo ya umwagiliaji, upatikanaji wa zana za kilimo, Rais Samia pia ameelekeza kuwahakikishia sera rafiki wawekezaji wa viwanda vya kuchakata pamba.
Aidha, amezielekeza wizara zingine za kisekta kushirikiana na Serikali mkoani Simiyu kuhakikisha mazao ya pamba na mbaazi yanapanda hadhi, ambapo mnada wa kwanza wa mbaazi utafanyika Ijumaa Bariadi.
Uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wilayani Busega, kutoka Ziwa Victoria na kusambazwa kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya, nayo ni historia nyingine kwa mkoa wa Simiyu. Mradi huo mkubwa utakuwa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa maji safi, salama na bora katika maeneo ya mkoa huo.
Kabla ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi, mapema leo Rais Samia atafungua mradi wa maji katika mji wa Lamadi na kuzungumza na wananchi wa Busega, kisha kuelekea Mwanza ambako atafanya uzinduzi rasmi wa Daraja la JP Magufuli, Kigongo – Busisi, ambalo ni la sita kwa urefu Afrika, lililojengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.
Rais Samia alifanya majumuisho rasmi ya ziara yake jana Jumatano katika mkutano mkubwa wa hadhara Bariadi, akitokea Maswa ambako pia alizungumza na umati wa maelfu ya watu kama ilivyokuwa maeneo mengine ya Nyakabindi, Mwanhuzi – Meatu, Itilima na Maswa, ambako alifika na kuzungumza na wananchi katika maeneo ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo au mikutano ya hadhara mkoani humo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED