Serikali kujenga madarasa mawili Mkowela

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:58 PM May 13 2025
Serikali kujenga madarasa mawili Mkowela

Baada ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, kudai kuwa Shule ya Msingi Mkowela iliyopo wilayani Tunduru inakabiliwa na uhaba wa madarasa na majengo chakavu, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imejibu kwa kueleza kuwa ina mpango wa kujenga madarasa mawili mapya katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa rasmi za halmashauri hiyo, ujenzi wa madarasa hayo unatarajiwa kugharimu takribani Shilingi milioni 48.

Hata hivyo, halmashauri imekanusha baadhi ya taarifa zilizotolewa na Ado Shaibu, ikidai kuwa si sahihi. Mfano, imeeleza kuwa shule hiyo ina walimu watano, tofauti na madai ya Ado kuwa walimu waliopo ni wanne.

Akitoa majibu ya ufafanuzi huo, Ado Shaibu amesema halmashauri imethibitisha hoja zake kuhusu changamoto za uhaba wa walimu na miundombinu mibovu shuleni hapo. Ameongeza kuwa ataendelea kufuatilia kwa karibu hali ya shule hiyo hadi pale itakapopata miundombinu bora na walimu wa kutosha.