Mkuu wa Tiba Jeshini, Meja Jenerali Amri Mwami, amesema Tanzania inaendelea kuaminiwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na mchango wake mkubwa katika ulinzi wa amani duniani.
Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Wakufunzi wa Maofisa Wanadhimu wa Umoja wa Mataifa (United Nations Staff Officers Training of Trainers – UNSO TOT),Amri alisema sifa hiyo imeifanya Tanzania kupewa nafasi ya kuendesha mafunzo muhimu ya kimataifa kuhusu ulinzi wa amani.
“Mafunzo haya yametolewa kwa mujibu wa miongozo mipya iliyofanyiwa maboresho na Umoja wa Mataifa. Kwa washiriki waliohitimu leo, wana jukumu la kwenda kutumia maarifa hayo kufundisha wenzao katika nchi zao ili kuboresha huduma za ulinzi wa amani zenye usalama na weledi wa hali ya juu,” alisema Amri.
Aliongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa katika operesheni za ulinzi wa amani duniani, jambo ambalo limeifanya kuheshimiwa na kuaminika zaidi katika nyanja hiyo.
“Sisi ni wachangiaji wakubwa wa amani, na kazi nzuri tunayoifanya inaonekana. Ndiyo maana mafunzo haya yamefanyika hapa nchini, kama ishara ya kuaminika kwetu katika suala la ulinzi wa amani,” aliongeza.
Akieleza kuhusu dhamira ya Umoja wa Mataifa, alisema jukumu lake kuu ni kuhakikisha amani inadumu kote duniani. Alibainisha kuwa pamoja na changamoto zinazojitokeza, juhudi za kurejesha na kuimarisha amani hufanyika kwa wakati.
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wakufunzi wa maofisa wanadhimu wa Umoja wa Mataifa, ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika misheni mbalimbali za kulinda amani.
“Mafunzo haya yanatolewa kwa mara ya kwanza hapa Tanzania, na pia kwa mara ya kwanza barani Afrika, yakitokana na mtaala mpya wa Umoja wa Mataifa. Hii ni mara ya pili kwa kozi hii kufanyika duniani, baada ya awamu ya kwanza kufanyika nchini Italia,” alisema Brigedia Jenerali Itang’are.
Naye Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, ambaye nchi yake imefadhili mafunzo hayo, alisema wanafarijika kushiriki katika juhudi za kuimarisha usalama wa kimataifa kupitia mchango wa Tanzania katika kulinda amani.
“Tunathamini uongozi na ushirikiano wa Tanzania katika kuendeleza amani duniani. Tuna imani kuwa wakufunzi waliopata mafunzo haya wataendelea kuimarika kitaaluma na kuchangia matarajio ya Umoja wa Mataifa ya dunia yenye amani na usalama,” alisema Balozi Emily
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo kutoka Umoja wa Mataifa, Kanali Ibrahim Abdul kutoka Nigeria, alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wakufunzi ili wanapopelekwa katika maeneo ya misheni ya kulinda amani, wawe na maarifa na mbinu zinazohitajika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yaliwaleta pamoja maofisa 22 na wakufunzi 7 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Ghana, Nigeria, Tanzania, Vietnam, Botswana na Zambia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED