Mawaziri wa Mawasiliano kutoka Tanzania na Kenya wamezindua rasmi maunganisho ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) wa Tanzania unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), na mikongo ya baharini ya Mombasa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (ICTA).
Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidigitali wa Kenya, Injinia William Kabogo Gitau, pamoja na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Jerry Silaa,. Mawaziri hao wamesema kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria na inaleta faida kubwa kwa mataifa yote mawili, hasa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika na kupunguza changamoto za kukatika kwa mtandao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Gitau amesema:
“Jambo la msingi ni ushirikiano wa dhati kati ya nchi zetu mbili. Ni muhimu kuhakikisha tunatunza miundombinu hii ya kimkakati ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababisha kukatika kwa umeme na mtandao. Pia tuendelee kuimarisha mahusiano yetu kwa manufaa ya pande zote.”
Kwa upande wake, Jerry Silaa alieleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya pamoja ya mawasiliano kati ya nchi washirika unapaswa kuwa wajibu wa pamoja.
“Kuna faida kubwa ya kuwa na maunganisho mengi ya mikongo ya mawasiliano. Hii husaidia kuwepo kwa mtandao wa uhakika, unaotegemewa hata wakati wa changamoto za kiufundi katika njia moja ya mawasiliano,” amesema Silaa.
Mkongo huo tayari umeanza kufanya kazi nchini Kenya, hatua inayowezesha huduma za intaneti na mawasiliano kusambaa kwa kasi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Maunganisho hayo yanaongeza uwezo wa Tanzania na Kenya kusambaza huduma za kidigitali, kuimarisha sekta ya TEHAMA, kuvutia uwekezaji na kusaidia kufanikisha malengo ya kidijitali ya kanda nzima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED