Wamiliki wa malori wataka ‘mwendokasi’ wasema wao ni watu wenye elimu

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 01:06 PM Nov 23 2024
Wamiliki wa malori wataka ‘mwendokasi’ wasema wao ni watu wenye elimu

WAMILIKI wa kati na Wadogo wa Malori Tanzania (TAMTOA) wamejitokeza KITUO cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), kuonyesha nia yao ya kuwekeza katika Mradi wa Usafiri wa Mwendokasi Dar es Salaam (BRT).

Viongozi na baadhi ya wanachama wa TAMSTOA wamezungumza leo na Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila wakimweleza nia yao ya kuwekeza kwenye mradi huo mkubwa wa usafirishaji Dar es Salaam ambao unaendelea kutekelezwa kwa awamu sita tofauti.

Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shaban  amesema wao ni watu wenye elimu ya kazi hivyo mchakato mrefu hawawezi, hivyo wanatamani kupewa utaratibu mzuri wa kufanikisha lengo lao.

Mjumbe wa Kamati kuu ya TAMSTOA, Josephat Pallangyo amesema anafikiri ni vyema utaratibu wa kuwekeza kwa hisa kama ilivyo kwa Benki ya CRDB  au NMB ungewekwa.

" Mabasi ya mwendokasi ni uwekezaji mkubwa lakini kwa utaratibu huo uliofanywa kwa benki, sisi kama wasafirishaji hatuna haja  ya kuwa na wawekezaji wa nje kwa kuwa uwezo tunao, management iwe nzuri tu, "amesema.

Mkurugenzi Kafulila aliwashauri kuandaa andiko lao jinsi gani wamejipanga kuwekeza pia uwezo wao ni kununua mabasi mangapi, na huduma nyingine ambazo zipo na wameziona kuwa ni fursa.

'Hadi  sasa mradi huo katika Awamu ya kwanza na pili zimekamiliki, hivyo wanaweza kuomba kuanzisha Awamu ya tatu na watapewa nafasi wakionyesha jinsi wanavyoweza kutoa huduma zao kulingana na utaratibu uliowekwa,"amesema.

Pia amewashauri kuanzisha kampuni ya umiliki wa pamoja, kisha wawekeze ambapo mtu atavuna faida iliyopatikana  kulingana na kiwango cha hisa anazomiliki, lengo la serikali ni kuhakikisha huduma nzuri zinapatikana kulingana na mradi husika. 

Septemba 02,2024 Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amesema hakuna haja ya kusubiri wawekezaji wa nje katika kupata mabasi  ya mwendokasi kwa huduma za mradi huo.