Yanga kuikaribisha Copco Kombe la FA

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:14 PM Nov 23 2024
   Yanga kuikaribisha Copco Kombe la FA
Picha: Mtandao
Yanga kuikaribisha Copco Kombe la FA

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la FA, Yanga wataanza kutetea taji hilo kwa kuwakaribisha Copco FC kutoka jijini, Mbeya katika hatua ya 64 bora wakati Simba itawavaa Kilimanjaro Wonderers, imefahamika.

Bingwa wa mashindano hayo hupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC yenyewe imepangwa kucheza na Iringa FC wakati Coastal Union itakutana na Stand United huku Moro Kids itawafuata Pamba Jiji FC ya Mwanza na Namungo FC itawaalika Tanesco katika hatua hiyo.

Katika droo iliyofanyika jana Singida Black Stars yenyewe itacheza dhidi ya Magnet, KenGold itakutana na Mambali FC, Tukuyu Stars itawafuata Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika huku KMC itajipanga kuwaalika Black Six na Tanzania Prisons itacheza dhidi ya Tandika United.

Mechi nyingine katika hatua hiyo itakuwa ni kati ya Tabora United dhidi ya Foysa Academy, Kagera Sugar itavaana na Rhino Rangers, Dodoma Jiji wao watapambana na Leo Tena huku Igunga United itasafiri kuwafuata Maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Isamhuyo ulioko Mbweni, Dar es Salaam.

Ratiba hiyo inaonyesha Mbeya City watacheza dhidi ya Mapinduzi FC, Green Warriors watakutana na Hausung, Geita Gold wao watapimana ubavu na Ruvu Shooting, Bigman FC itawaalika Soccer City na Cosmopolitan itachuana na Nyota Academy.

Meneja Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema jana mechi za raundi ya tatu zitachezwa kati ya Desemba 6 na 8, mwaka huu.

"Tunazitakia maandalizi mazuri timu zote zilizofuzu hatua hii, tunaamini kila timu itajiandaa kufanya vizuri katika mashindano haya, tunatarajia ushindani utaongezeka kwa sababu hakuna timu itakayokuwa tayari kuondolewa kirahisi katika michuano hii," alisema Kizuguto.