IDADI ya watu waliofariki kutokana na mafuriko yaliyoikumba nchi Afghanistan mwishoni wiki hii imefikia watu 84 huku majengo na mali nyingine vikiharibiwa kwa maji.
Awamu hiyo mpya ya mvua kubwa na mafuriko imeziathiri Wilaya nne katika Jimbo la Faryab, ambapo jana Jumamosi watu 66 walithibitishwa kupoteza maisha, watano wamejeruhiwa na wengine 8 hawajulikani walipo.
Msemaji wa Gavana wa Jimbo hilo wa kundi la Taliban, Esmatullah Moradi amesema watu wengine 18 walifariki siku ya Ijumaa huku jumla ya nyumba 1,500 zimeharibiwa kwa mafuriko na mamia ya hekari za mazao zimesombwa.
Idadi hiyo ya vifo inafuatia nyingine iliyotolewa wiki iliyopita na shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP ambayo ilionesha watu 300 wamekufa nchini Afghanistan tangu kuanza kwa msimu wa sasa mvua.
Majimbo ya Ghor na Baghlan ndiyo yameshuhudia uharibifu usio mfano kutokana na mvua hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED