WATU saba wamefariki dunia baada ya bajaji waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mpemba, Tunduma wilayani Momba, mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustine Senga, alisema jana ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:15 usiku, wakati dereva wa bajaji yenye namba za usajili MC 783 DUF akijaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake.
Alisema dereva wa bajaji hiyo, Emmanuel Hakimu, ambaye ni mmoja wa watu saba waliofariki dunia katika ajali hiyo, alikuwa akitokea eneo la Mpemba kwenda mjini Tunduma.
Alisema bajaji hiyo iligongana na lori aina ya Scania lenye namba T 958 BCS na kwamba watu watano walifariki dunia papo hapo na wengine wawili, akiwamo mtoto wa miaka miwili, Isack Mambwe, walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu.
Kamanda Senga aliwataja wengine waliofariki dunia kuwa ni Rehema Christopher (25) mkazi wa Msongwa, Festo Mambwe (57) mkazi wa Mbeya, Rosemary Njema (44) mkazi wa Ipito mjini Tunduma na Milembe Siyantemi (36) mkazi wa Kapele, wilayani Momba.
Kamanda Senga alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku wakiendelea kumtafuta dereva wa lori ambaye alitoweka baada ya tukio hilo.
“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Tunduma. Chanzo cha ajali hii bado tunakichunguza ikiwa ni pamoja na kumsaka dereva wa Scania," alisema.
Kamanda Senga aliwataka madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kujenga tabia ya kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari na kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wote ili kuzuia ajali zinazoepukika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED