GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewahakikishia Watanzania kuwa mifumo yote ya malipo inayohusisha akaunti za serikali, benki na simu za mkononi iko salama na madhubuti.
Kutokama na hali hiyo, amesema mifumo hiyo inawezesha kufanyika miamala kiurahisi na usalama.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa ziara ya baadhi ya viongozi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushukuru mchango wa benki hiyo katika ulipaji kodi, Gavana Tutuba aliwataka wananchi kuhakikisha wanatumia mifumo rasmi ya malipo ili kuhakikisha fedha zao zinaingia salama katika akaunti zinazohusika.
“Mifumo yetu iko imara na inafanya kazi bila changamoto. Ukilipa kwa hundi, akaunti ya benki au kutoka akaunti kwenda kwa simu, kila njia iko salama. Akaunti zote za serikali ziko salama na fedha zinaingia moja kwa moja bila vikwazo vyovyote,” alisema Tutuba.
Pia alisema BoT inasimamia akaunti zote za serikali pamoja na benki na pia inahakikisha usalama wa fedha zilizohifadhiwa kwenye kampuni za simu.
Kwa mujibu wa Tutuba, timu za kitaalamu za ufuatiliaji wa uhalifu mtandaoni zinafanya kazi saa 24 kuhakikisha hakuna vitisho vya usalama vinavyoathiri mifumo hiyo.
“Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa mifumo inafanya kazi muda wote na hata wale wanaojaribu kudukua wanashindwa kwa sababu tunadhibiti kila kitu kwa wakati,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Dinah Edward, alisema mamlaka hiyo inatarajia kukusanya kodi ya Sh. trilioni 15.27 kuanzia Januari hadi Juni, mwakani huku Desemba, mwaka huu, ikiwa na lengo la kukusanya Sh. trilioni 3.46.
Edward alisema lengo hilo ni sehemu ya mpango wa kufanikisha ukusanyaji wa Sh. trilioni 31.05 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Mpaka kufikia Novemba, mwaka huu, TRA imekusanya Sh. trilioni 12.94 sawa na asilimia 105.1 ya malengo ya kipindi hicho au asilimia 41.67 ya lengo la mwaka mzima.
“Tunatarajia kuweka rekodi mpya ya ukusanyaji kodi lakini mafanikio haya yanahitaji ushirikiano mzuri kati yetu, walipakodi na wadau mbalimbali,” alisema.
Edward alibainisha kuwa TRA imeweka mikakati ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji kodi kwa kuimarisha mifumo ya kielektroniki na kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo BoT, ili kuhakikisha malengo yanafikiwa.
USHIRIKIANO BOT, TRA
Gavana Tutuba alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya BoT na TRA kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.
“Tunashirikiana kikamilifu kuhakikisha kila malipo yanafanyika kwa njia salama na rahisi,” alisema.
Aidha, aliipongeza TRA kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 105 kwa kipindi cha miezi sita iliyopita, hatua aliyosema ni ishara ya jitihada madhubuti za mamlaka hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED