Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Salumu Mwalimu, ameahidi kuwa endapo wagombea wa chama hicho watapata ridhaa ya kuongoza serikali za mitaa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hakuna mwananchi atakayelazimishwa kutoa fedha kwa huduma za kugongewa mhuri au kupata nyaraka mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Kagongwa, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mwalimu alisisitiza kuwa vitendo vya kuomba rushwa hata ya kiwango cha Sh. 5,000 au 10,000 vitachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwavua wanachama waliokiuka kanuni za chama.
Mwalimu alieleza kuwa baadhi ya wananchi wamekosa huduma muhimu za kijamii kutokana na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa. Aliongeza kuwa CHADEMA imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bila gharama zisizo za lazima, na akatoa wito kwa wananchi kuichagua CHADEMA ili kumaliza changamoto hizo.
“Ofisi za wenyeviti wa mitaa hazipaswi kuwa chanzo cha mapato. Mwananchi yeyote atakayeombwa fedha kwa huduma kama mhuri wa nyaraka apeleke taarifa katika ofisi za chama ili hatua zichukuliwe,” alisema Mwalimu.
Mwalimu alionya dhidi ya tabia ya vijana kutochukulia uzito uchaguzi wa serikali za mitaa. Alisema uchaguzi huu una umuhimu mkubwa kuliko uchaguzi mkuu kwa sababu huduma nyingi muhimu, kama upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), hati za kusafiria, na akaunti za benki, zinategemea mamlaka za serikali za mitaa.
“Vijana wengi wanapuuza uchaguzi huu kwa sababu wanajali tu kupata vitambulisho vya wapiga kura, lakini wanapoteza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi. Hii ni haki yao ya kikatiba, na tunawahimiza kujitokeza kwa wingi Novemba 27 kuchagua viongozi bora,” alisisitiza.
Mwalimu alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura na kuchagua viongozi wenye maono na uwezo wa kusimamia maendeleo yao. Alisisitiza kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ndio msingi wa kuunda serikali bora ya kitaifa, hivyo wananchi hawapaswi kuupuuza.
“Uchaguzi huu ndio unaotupatia dira ya kupata viongozi bora wa kitaifa. Tuoneshe uzalendo kwa kujitokeza kupiga kura na kuleta mabadiliko tunayotaka,” alisema Mwalimu.
Katika mkutano huo, wagombea wa CHADEMA walisisitiza dhamira yao ya kuleta mabadiliko na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila ubaguzi au mzigo wa gharama zisizo za lazima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED