WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ameushukuru Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia (SFD), kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo hususan sekta za maji, afya, nishati na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Dk. Nchemba alitoa shukrani hizo juzi alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa SDF, Sultan Al-Mashard, Kando ya Mkutano wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji, lililofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia.
Dk. Nchemba aliyeambatana na mawaziri wenzake wawili katika kikao hicho, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema ushirikiano wa Saudi Arabia na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 40 sasa, umekuwa wa mfano.
Aliitaja baadhi ya miradi iliyoleta mageuzi makubwa katika jamii ya Tanzania kuwa ni pamoja na ukarabati wa mradi wa maji mkoani Mara uliogharimu Dola la Marekani milioni 15, ujenzi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe uliogharimu Dola za Marekani milioni 25 na na ujenzi wa barabara za vijijini awamu ya pili Zanzibar wenye thamani ya Dola milioni nne.
Miradi mingine kwa mujibu wa Waziri Nchemba ni ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja-Zanzibar uliogharimu Dola milioni 15 na kushirikiana na wadau wengine kufadhili mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa Kilovolti 220 kuanzia Benako hadi Kyaka wa thamani ya Dola milioni 105.4.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Nchemba aligusia utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ya kimkakati inayoendelea nchini Tanzania ukiwamo wa reli ya kisasa (SGR), ambao alisema utakapokamilika utakuwa kichocheo kikubwa cha biashara na uchumi katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Waziri wa Viwanda na Biashasra, Dk. Selemani Jafo na Dk. Mkuya, walisema ushiriki wa SDF katika ujenzi wa miradi ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania utachochea maendeleo ya nchi.
Al-Marshad alisema mfuko huo uko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kutokana na uhusiano imara uliopo kwa faida ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Alipongeza hatua kubwa zinazochukuliwa na serikali katika kutekeleza miradi muhimu kwa maendeleo ya nchi akiitaja reli ya kisasa inayojengwa kwamba itachochea na kukuza biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo katika eneo la mradi.
Katika kikao hicho Tanzania na SDF zilikubaliana kuunda timu ya wataalam watakaopitia, kuchambua na kuchakata miradi mbalimbali ambayo mfuko huo utatoa fedha ili kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED