MJUMBE wa Baraza la Ushauri la Wazee nchini Joseph Mbasha amesema kuelekea mwaka 2050 ni muhimu kama nchi kuamua kuwa kinara wa mfuko wa hifadhi ya jamii maalum kwaajili ya wazee ili kuhakikisha kundi hilo linapata mahitaji na stahiki zao muhimu.
Akitoa maoni yake wakati wa kupitia rasimu ya kwanza ya dira ya maendeleo ya taifa 2050 leo Jijini Dar es Salaam, mzee huyo amerejea takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) linalosema kuwa kufikia mwaka 2050 duniani kote idadi ya Wazee inaweza kufikia Bilioni 2.1.
Mzee Mbasha amesema ni muhimu kujiandaa mapema na ongezeko hilo la wazee kwa kuwatengenezea mazingira rahisi yatakayohakikisha ustawi wao unaimarika.
"Nihimize pia maandalizi mazuri kwa vijana wa sasa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, kama sehemu ya kuondokana na ombwe kubwa la wazee wa baadae wasiokuwa wameandaliwa vyema," amesema.
Wakati huo huo, wazee hao wameshauri kuwa kuelekea 2050 ni muhimu kuunda na kuimarisha mabaraza ya wazee kwenye ngazi zote za kiutawala kama sehemu ya kutunza na kulinda maadili ya Tanzania dhidi ya tamaduni mbalimbali za kigeni zinazosambaa kote duniani.
"Kuundwa kwa mabaraza hayo kutasaidia pia kuondoa manyanyaso mbalimbali wanayokutana nayo wazee kutoka kwa vijana na wanajamii ambao hawakuandaliwa vyema kuishi kulingana na maadili tarajiwa," amesema.
Mzee huyo amesema mabaraza hayo yaliyoimarishwa na kuwezeshwa yatasaidia pia kurejesha misingi ya familia kwa kuhakikisha familia zinatimiza majukumu yake kikamilifu ikiwemo kutoa matunzo stahiki kwa wazee.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED