Wameng’ooka KIA sawa, uwanja unalindwaje?

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 02:38 PM May 19 2024
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mohbare Matinyi.
Picha: Maktaba
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mohbare Matinyi.

NAKUBALIANA na hoja ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mohbare Matinyi, kuhusiana na uamuzi wa kuwaondoa wananchi katika ardhi inayomilikiwa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Pamoja na kukubaliana huko, nina maswali hayaishi kichwani.

Hakuna ubishi kwamba kaya zilizoko ndani ya eneo hilo la ardhi ya KIA ni 1,712 za vijiji vinane vya mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Kama hoja ni kuwaondoa kwa sababu ya vumbi kubwa la upepo wa kisulisuli linalotimka, kuathiri miruko na utuaji wa ndege kiasi cha ndege kushindwa kutua na kwenda nchi jirani, je, tatizo litakuwa limekwisha?

Nani alifumba macho, akawaacha wakaingia katika ardhi hiyo na kuwaacha wakajenga makazi, wakaanzisha shughuli za kiuchumi kama ufugaji na kilimo ili alaumiwe?

Hilo eneo kwa sasa litalindwaje ili kutoruhusu wananchi, hasa wa jamii ya kigugaji ya Kimasai kutoingiza mifugo yao na kuendelea kuathiri utoto wa asili na mazingira yake.

Miongoni mwa athari pia ni shughuli za kibinadamu kusababisha kuharibika kwa uoto wa asili kwa kukata miti, majani na kulisha mifugo na pia kusababisha serikali kushindwa kutekeleza mpango wake mahususi kwa ajili ya kuendeleza uwanja huu.

Taarifa ya serikali inaeleza kwamba uwanja wa KIA ulivamiwa na wananchi wa wilaya za Hai (Kilimanjaro) na Arumeru (Arusha) kati ya mwaka 2007 hadi 2010.

Lakini taarifa hiyo hiyo, inasema uwanja huo ulianza kumilikiwa na serikali mwaka 1969 wakati huo ukiwa chini ya Pori Tengefu la Sanya Lelatema, lililokuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 800.

Katika eneo hilo, inaelezwa kuwa serikali ilitenga kilomita za mraba 110 kutoka kwenye hizo 800 mahususi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo na baadaye na eneo lilipimwa rasmi mwaka 1989 kwa ramani iliyokuwa na namba E 5255/18 kisha ukasajiliwa na kupewa namba 231264 na hatimaye hati ilipotoka ilianza kumilikiwa ikiwa na hati 22270.

Wavamizi wanatoka vijiji vinne vya wilaya ya Arumeru ambavyo ni Kaloleni, Samaria, Malula na Majengo Kati na upande wa wilaya ya Hai, kuna vijiji vinne ambavyo ni Sanya Station, Tindigani, Chemka na Mtakuja.

Katika taarifa hiyo ya serikali, wilaya ya Arumeru wananchi wamelipwa fidia zaidi ya Sh. bilioni 4.042, wakati wilaya ya Hai wamelipwa Sh. bilioni 7.27 zilizojumuisha fidia ya majengo, mazao ya kudumu, posho ya makazi, posho ya usafiri, posho ya usumbufu na posho za makaburi.

Mpaka kufikia Mei 14, mwaka huu, wananchi 46 pekee ndio ambao bado hawajalipwa malipo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukosa akaunti za benki, majina kutofautina yaliyoko katika taarifa za malipo na yaliyoko benki.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, kuna tatizo la kukosekana kwa uthibitisho wa mirathi kwa wananchi wanaotakiwa kulipwa fidia na baadhi ya wananchi kufungua mashauri ya madai Mahakama Kuu, kupinga ulipaji unaoendelea.

Haiingii akilini unawaacha watu wanavamia uwanja, wanajenga makazi ya kudumu, halafu ndipo serikali inaamka. Hivi hamkuwaona wakati wanajenga ndani ya uwanja?

Nakumbuka Agosti, 2014 kamati ya usuluhishi iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (wakati huo), kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa vijiji hivyo vinane, ilishindwa kutekeleza jukumu hilo baada ya wanavijiji hao kukataa wazo la kutaka kuwekwa upya kwa alama za mipaka ya ardhi.

Wakati huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
 Makazi, alikuwa Prof. Anna Tibaijuka, ambaye alipambana kufa na kupona kuwahamisha katika makazi yao wananchi hao bila mafanikio. 

Hoja ya Tibaijuka ilikuwa kupisha upanuzi wa uwanja huo kabla ya serikali kutumia nguvu. Leo Rais Samia Suluhu Hassan kafanikiwa kutumia diplomasia, kuwalipa fidia na wameondoka kwa hiari. Tunamshukuru kwa wema huo.

Sasa, kama ndivyo, ili kubakiza hai malengo ya uendekezaji wa uwanja wa KIA, ni lazima maeneo yake yadhibitiwe kwa namna yeyote ile, yasiendelee kuvamiwa.

·         Godfrey Mushi, ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa simu namba 0715 545 490 au barua pepe: ghandsome79@gmail.com