Ni wakati mwafaka kwa wanaume kupaza sauti dhidi ya manyanyaso

Nipashe
Published at 08:44 AM Dec 13 2024
Ni wakati mwafaka kwa wanaume kupaza sauti dhidi ya manyanyaso
Picha:Mtandao
Ni wakati mwafaka kwa wanaume kupaza sauti dhidi ya manyanyaso

VITENDO vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikishamiri mwaka hadi mwaka ndani ya jamii na hata kuacha maumivu yasiyoisha kwa baadhi ya watu. Miongoni mwa vitendo hivyo ni ukatili wanaofanyiwa wasichana na wavulana wa kazi dhidi ya mabosi wao, vipigo kwa wanawake kutoka kwa wenzi wao na hata vifo, ukeketaji na mauaji ya vikongwe.

Kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo, wadau wa haki za binadamu wamekuwa wakijitokeza hadharani na kulaani hata kuweka mikakati ya  kuzuia kuendelea kutokea. Moja ya mambo yaliyofanikiwa na wanaharakati hao ni kutungwa kwa sheria ya makosa ya kujamiiana, ambayo wanaokutwa na hatia adhabu yao ni kifungo cha miaka 30 jela.   

Kwa muda mrefu, sehemu kubwa ya jamii imekuwa ikidhani kuwa wanaofanyiwa vitendo hivyo vya kikatili ni wanawake na watoto na lawama nyingi kuelekezwa kwa kinababa. Ukweli ni kwamba wako baadhi ya wanaume wanaofanyiwa vitendo hivyo na wenza wao na wakati mwingine kwa kushirikiana na watoto. Moja ya mifano ya matukio hayo ni wanawake kuwakimbia waume zao huku wakiondoka na mali zote na kuwaacha watupu.      

Wanaume hao wamekuwa wakinyimwa unyumba, kupigwa na kunyanyaswa na wenza wao huku wakishindwa kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo. Sababu  kubwa inayowafanya kukaa kimya au kutoripoti matukio hayo ni kudhani kwamba wanaweza kudharauliwa na jamii. Hali hiyo imewafanya wengi kukaa na machungu moyoni huku wakipata maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, msongo wa mawazo na tatizo la afya ya akili. 

Unyanyasaji huo dhidi ya wanaume umekuwa ukitokana na baadhi yao kuporomoka kiuchumi au mwanamke kuwa na uwezo wa kiuchumi dhidi ya mwanamume. 

Matokeo yake wanaume wamekuwa wakidharauliwa na hata kupewa majina kama ‘mwanamume suruali’ au ‘kula kulala’.    

Siku hizi, ni jambo la kawaida kumkuta mwanamume barabarani akizungumza peke yake huku hali yake ikiwa dhaifu. Miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo ni kuporomoka kiuchumi, kukosa kazi au kuachishwa kazi ambayo ilikuwa ikimpatia riziki yake na familia kwa ujumla. Hapo pia manyanyaso dhidi yake ndani ya nyumba kutoka kwa mwenza na familia yanaibuka. 

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimewataka wanaume kuacha kulia majumbani wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wake zao, badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya kisheria yakiwamo madawati ya jinsia. Chama hicho wakati wa mdahalo wa Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia juzi jijini Dodoma, kilibainisha kwamba bado kuna wanaume wanafanyiwa vitendo vya kikatili lakini wanaishia kulia ndani ya nyumba, hivyo kutakiwa watoe taarifa ili wapatiwe msaada wa kisheria. 

Wahenga wanasema ukimya wako umaskini wako na kimya chako ni mauti yako. Kwa mantiki hiyo, wanaume wanaonyanyaswa kuendelea kunyamazia vitendo hivyo kuna madhara makubwa dhidi yao. Ndiyo maana kumekuwa na matukio ya baadhi ya wanaume kuchukua  uamuzi mgumu kama kuwaua wenza wao na kisha kujiua kutokana na kukaa na mambo moyoni bila kuyaweka bayana.  

Mtindo au tabia ya wanaume kukaa kimya dhidi ya unyanyasaji wanaofanyiwa na wake zao na wakati mwingine kushirikiana na watoto, umepitwa na wakati, hivyo ni wakati mwafaka kwao kupaza sauti pindi wanapokutana na mambo kama hayo ili kuokoa maisha yao na kuwaepusha na madhara yanayoweza kuwapata.