KILA msimu kunakuwa na makosa ya baadhi ya waamuzi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kwa namna walivyoanza msimu huu kuna uwezekano mkubwa ukatia fora.
Hata nusu msimu bado, lakini kumekuwa na malalamiko lukuki ya maamuzi ya hovyo, kwa baadhi ya waamuzi ambayo bila kupepesa macho 'yanaunajisi' mpira wa Tanzania.
Kuna kile kinachoelezwa kuwa makosa yanayofanywa na baadhi ya waamuzi ni ya kibinadamu, lakini ukiangalia kwa jicho la tatu unaweza ukapinga kuwa si ya kibinadamu kama inavyoelezwa kwani ni makusudi.
Bila kuitaja timu yoyote, lakini mara nyingi utakuta ni timu hiyo hiyo au hizo hizo ndizo zinazonufaika zaidi na makosa yao ya kibinadamu kupitia kwa waamuzi.
Tunavyotambua maana halisi ya makosa ya kibinadamu katika soka ni yale ambayo mwamuzi ni vigumu kuyabaini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutokea kwa haraka zaidi kutokana na kasi ya mpira, lakini pia kila mmoja kuwa na mapungufu yake kama mwanadamu.
Lakini ukiona kila siku waamuzi hao hao wanafanya makosa yale yale kwa timu hiyo ama hizo hizo, basi dhana ya makosa ya kibinadamu hapo haipo, zaidi ya kusema kuna timu haitendewi haki na nyingine kubebwa.
Tulitegemea kama ni makosa ya kibinadamu, basi hata timu ambazo zinanufaika na zenyewe itokee siku ziathirike na makosa hayo hayo, yaani karibuni timu zote zifaidike dhidi yao, hayo ndiyo makosa ya kibinadamu tuyajuayo Nipashe.
Lakini makosa ya baadhi ya waamuzi wa Tanzania siku zote yanainufaisha timu moja zaidi au chache, hizo ndizo kila siku zinapata faida ya makosa hayo na zingine kazi yao ni kulia tu kwa kuonewa, hapo ni kuzifinyanga Sheria 17 za Soka.
Hapa ndipo wasiwasi wetu unapoanza kuja hasa kutokana na kauli baadhi ya mashabiki wanaposema bingwa wa msimu huu tayari ameshaandaliwa, ingawa hatutaki kuamini hivyo.
Lakini kingine kinacholeta wasiwasi ni waamuzi wanaoharibu ama kwa lugha yao, wenye makosa ya kibinadamu ni wale wenye majina makubwa na wazoefu wa kuchezesha mechi kubwa kubwa tu.
Ukitazama katika michezo ya Ligi Kuu, kuna waamuzi wengi wapya, wanaume pamoja na kinadada ambao ni chipukizi, lakini wamekuwa wakichezesha vizuri michezo yao tofauti na hao wanaotajwa ni wazoefu.
Cha ajabu waamuzi wanaotegemewa ambao ni wazoefu, ukimuondoka, Ahmed Arajiga, wamekuwa wakifanya makosa mengi kwenye uchezeshaji wao kiasi cha mashabiki kujiuliza maswali mengi.
Inawezekana hivi karibuni Kamati ya Bodi ya Ligi ambayo zamani ilifahamika kama Kamati ya Saa 72, ikakaa kwa ajili ya kupitia mwenendo wa michezo yote, lakini hilo lilipaswa kufanywa mapema zaidi, ili kuwa fundisho kwa wanaopewa nafasi ya kuchezesha mechi zinazofuata.
Tunachotaka sasa TFF na Bodi ya Ligi itoe adhabu kali kwa waamuzi wote ambao wameonekana kufanya makosa ambayo hayastahili hata kuwa na Video ya Usaidizi, VAR, ili kuyang'amua.
Tunatoa msisitizo huo kwa kuwa tuendapo tunaona sasa utafika wakati hata mashabiki wachache wanaojitokeza viwanjani wataona hakuna haja tena ya kwenda kwani tayari timu itakayoshinda inajulikana.
Hii itakuwa ni hasara kwa kila mtu, kuanzia TFF yenyewe, Bodi ya Ligi, klabu, wadhamini wa klabu na hata waliowekeza kwenye kurusha matangazo.
Sisi tunasikitika kuona klabu zikiwa zimewekeza kununua wachezaji wazuri na ghali kutoka nchi mbalimbali na kuifanya ligi yetu kuvutia, baadhi ya waamuzi wao wako kazini kushusha kiwango cha soka na kutaka kuturejesha kule kule tulipotoka kwa kutofahamu au kwa maslahi yao binafsi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED