BoT kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 08:20 AM Oct 27 2024
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Picha:Nipashe Digital
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetangaza kuondoa noti mbalimbali za zamani kwenye mzunguko na kuwataka Watanzania kubadilisha kupitia ofisi za benki hiyo na benki za biashara kuanzia Januari, mwakani.

Noti hizo ni ya Sh. 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003 na noti ya Sh. 500 iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 858 la Oktoba 11, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba,  ubadilishwaji unatarajiwa kuanza Januari 6 hadi Aprili 5, mwakani, kupitia ofisi za BoT na benki zote za biashara, kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawa na kiasi kilichowasilishwa.

Aidha, alisema matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia Aprili 6, 2025.

“Baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote duniani na benki hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko,” alisema.

Alitoa rai kwa wananchi wote wenye akiba ya noti hizo kuzibadilisha au kuziwekea amana kwenye benki yoyote ndani ya muda huo.