SERIKALI mkoani Shinyanga, imewataka viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU), kwenda kujifunza katika Chama Kikuu cha Ushirika (KACU) namna ya uendeshaji wa ushirika na ulipaji wa madeni wanayodaiwa ili kupata sifa ya kuendelea kukopesheka na taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo na Kilimo (TADB).
Mndeme ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa ulipaji wa malipo ya pili ya zao la pamba kwa wakulima waliouza pamba kwa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) zaidi ya kilo milioni 5.175 katika msimu wa 2023/2024 na kwa kilo moja watalipwa Sh.36 sawa na zaidi ya Sh. milioni 186.316 ambazo zimetolewa kwao.
Amesema, KACU imewekeza kulipa malipo ya pili kwa wakulima wake waliokiuzia pamba msimu 2023/2024 na kulipa madeni yote waliyokopa kwenye Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa asilimia 100 huku SHIRECU ikidaiwa Sh. bilioni 9 na kukosa sifa ya kukopesheka na taasisi za kifedha hali inayosabisha kushindwa kukua kimaendeleo.
“Niwapongeze KACU kwa kumaliza mikopo yote mliyokopa kwenye taasisi za kifedha na sasa mnalipa malipo ya pili kwa wakulima wenu wa pamba, niwaombe viongozi wa SHIRECU kulipa madeni yote mnayodaiwa ya Sh. bilioni tisa na kuja kujifunza namna ya uendeshaji wa ushirika” ameongeza Mndeme.
Mwenyekiti wa KACU, Tano Nsabi amesema, msimu wa kilimo wa 2023/2024 walikopa mkopo wa muda mfupi wa Sh. bilioni 9 na kununua pamba na kuchambua jumla ya kilo milioni 6 za pamba mbegu, kati ya kiasi hicho walitumia Sh. bilioni 5.962 sawa na asilimia 62.22 ya fedha waliyokuwa wamekopa.
Amesema, baada ya mauzo ya nyuzi na mbegu wamefanikiwa kurejesha kwa asilimia 100 mkopo wote waliotumia pamoja na riba yake ya jumla ya Sh.bilioni 6.121 na sasa wanajipanga kukopa tena fedha za kununua pamba msimu ujayo zaidi ya kilo milioni 6 na faida itakayopatikana watalipa pia malipo ya pili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED