Majaliwa: Rais Samia ametuheshimisha Ruangwa

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 05:40 PM May 04 2025
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
PICHA: MPIGAPICHA WETU
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kuleta maendeleo wilayani Ruangwa mkoani Lindi, akieleza kuwa thamani aliyowapa wananchi wa Ruangwa italipwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.


Waziri Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, ameyasema hayo leo mkoani humo, akieleza kuwa awali changamoto zilikuwa ni nyingi Wilayani Ruangwa ila kwasasa serikali imezitatua, na kwamba thamani ya jitihada hizo inatambulika na watu wote bila kujali itikadi zao za siasa.

Pia amemshukuru Rais Samia kwa kumchagua kama msaidizi wake Mkuu katika shughuli za serikali miongoni mwa wengine 789, akieleza kuwa jambo hilo linatokana na hekima alizozipata kutoka kwa wazee, kina Mama na vijana wa Ruangwa.

1

“Ni muhimu tukamtambua Rais Samia kwa kitendo chake cha kumchagua Mwanaruangwa mmoja kati ya 789 kumsaidia kazi yeye sio jambo dogo ni hekima zenu wazee, vijana na akinamama. Kama leo Ruangwa tunakuwa na shida tunasema tumepata, huyo aliyetoa tunamuachaje? Upendo alionao, heshima anayoendelea kutupa ni muhimu tukaithamini na sisi,” amesema Majaliwa.

Amesisitiza umuhimu wa kusimamia kikamilifu dhamira ya kumlipa kupitia boksi la kura wakati wa uchaguzi mkuu, ambako wananchi hao pia wameahidi kumpa kura Majaliwa ambaye ametoa ahadi za kuendelea kuchapa kazi zaidi ikiwa watamchagua kwa mara nyingine kwenda kuwawakilisha Bungeni kwa miaka mitano ijayo.

“Nitakuwa mchapakazi zaidi ya sasa, nitawachapia kazi kwelikweli zaidi ya sasa na kwahiyo tuendelee kuhamasishana kwenye maeneo yote, wazee kwa vijana na wakinamama wakati utakapokaribia tujitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na sisi wana Ruangwa tunajua tunaenda kumpigia nani kura na wanachama wa CCM tunalojukumu la kusema namna tulivyotekeleza ilani katika wilaya hii,” amesema Majaliwa.

 Pia Majaliwa ametaja tafanikio yaliyopatikana katika eneo hiyo ikiwemo miradi ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari zilizotekelezwa ndani ya miaka minne ya Rais Samia, sambamba na ile ya uchimbaji visima kila Kijiji pamoja na utekelezaji wa mradi wa Maji wa Vijiji 54 vya Ruangwa na Nachingwea.