Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kama Mkoa wa Shinyanga ungekuwa nchi inayojitegemea, basi Tanzania ingelazimika kuja kuikopa fedha. kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali uliopo mkoani humo.
Masoud ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, ametoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Town mjini humo.
Amesema pamoja na mkoa huo kuwa na utajiri mkubwa wa madini,lakini hadhi yake haiendendani, sababu bado umedumaa kimaendeleo, jambo ambalo amedai kuwa ni matokeo ya uongozi mbovu na usiojali maslahi ya wananchi.
“Kwa utajiri wa madini uliopo Shinyanga, kama ingekuwa nchi huru, Tanzania ingekuwa inakuja kukopa fedha. lakini hali ya sasa imedumaa kwa maendeleo kutokana na uongozi mbovu,” amesema Masoud. “Leo eti mnajisifia kujenga Uwanja wa Ndege, mmechelewa ,Uwanja huo ulipaswa kuwepo zamani sana, sababu ni mkoa ambao ni tajiri,”ameongeza.
Aidha, amewataka wananchi wa Shinyanga kwamba, katika uchaguzi mkuu ujao kuwa siku ya kupiga kura wasifanye makosa, bali waiadhibu CCM kwa kuwachagua wogombea ambao wanatokana na ACT-Wazalendo ili wawaletee maendeleo ya kweli.
Katika hatua nyingine, amesema kwamba wao Chama cha ACT-Wazalendo, hawawezi kususia uchaguzi Mkuu, bali watashiriki licha ya kuwapo kwa mapungufu kwenye mfumo wa uchaguzi, na kwamba uchaguzi ndiyo uwanja wa mapambano wa kuiondoa CCM madarakani.
"ACT-Wazalendo tutashiriki uchaguzi, kwa sababu huo ndiyo uwanja rasmi wa mapambano wa kidemokrasia wa kuitoa CCM madarakani, na huu ndiyo msimamo wetu kama Chama," amesema Masoud. Aidha, amesema kwamba kwa uzoefu walionao, Chama Cha Mapindizi (CCM) siyo wa kuwasusia uchaguzi sababu hakuna ambacho kitakacho badilika, bali watapambana nao hivyo hivyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, amesema wameanza ziara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, mbayo imelenga kutoa mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho katika kuelekea Uchaguzi Mkuu, pamoja na kuimarisha uhai wa chama. Katika Mkutano huo wa hadhara, ACT-Wazalendo ilipokea wanachama wapya 26, waliotoka vyama mbalimbali vya siasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED