Wananchi wa kijiji Luhangano kata ya Mputa wilaya ya Namtumbo wameiomba serikali kuona umuhimu wa kuwasaidia kuwapelekea huduma ya nishati ya umeme katika zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na mbunge wa jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa mwishoni mwa wiki.
Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na diwani ya kata ya Mputa, Swalehe Moto kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa zahanati hiyo na kuwakabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 14.9 ambavyo vitasaidia kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho ambao awali walikuwa na tatizo kubwa la kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji vingine vinavyotoa huduma ya afya.
Moto ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maendeleo kata ya Mputa alisema kuwa pamoja na kwamba serikali imesaidia upatikanaji wa huduma mbalimbali za maendeleo bado kuna tatizo la nishati ya umeme katika zahanati ya kijiji hicho hivyo aliiomba serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuona namna ya kuwasogezea huduma hiyo kwenye zanahati ili waganga pamoja na wahudumu wa afya waweze kuwahudumia wagonjwa kwa weledi zaidi.
Alisema kuwa mbunge wa jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa amekuwa ni mwakilishi mzuri kwenye bunge la jamhuri ya muungano wa tanzania kwa kupigania maendeleo ya jimbo hilo kwani kwa upande wa kata ya mputa ina shule za msingi tano na sekondari moja ambayo inawafunzi wa kidato cha kwanza hadi kidato cha sita ambazo kwa juhudi za mbunge wao pamoja na serikali zimefanyiwa ukarabati mkubwa wa miundo mbinu ya madarasa pamoja na matundu ya vyoo.
Ofisa mtendaji wa kijiji cha Luhangano, Veronia Tembo alisema kuwa zahanati ya kijiji chao bado inahitaji kupatiwa vifaa tiba zaidi kwani eneo hilo lipo mbali na makao makuu ya kata na alimweleza mbunge kuwa iko haja ya kuona umuhimu wa kuwa karibu zaidi na kijiji hicho ambacho kinahitaji zaidi kutatuliwa changamoto zinazowakabili licha ya kuwa kijiji hicho kina maji ya mtiririko ambayo yanatosheleza baada ya mbunge kusaidia kutatua tatizo la maji ambalo lilikuwa linawakabili wananchi kwa muda mrefu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED