Stendi,Soko Kuu zasafishwa, DAS Arusha aongoza kampeni ya mazingira safi

By Getrude Mpezya , Nipashe Jumapili
Published at 01:36 PM Jun 01 2025
Stendi,Soko Kuu zasafishwa, DAS Arusha aongoza kampeni ya mazingira safi
Picha: Mpigapicha Wetu
Stendi,Soko Kuu zasafishwa, DAS Arusha aongoza kampeni ya mazingira safi

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha,Jacob Rombo, ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Arusha kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Kauli hiyo imetolewa katika uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ngazi ya Mkoa wa Arusha, ambapo shughuli za usafi zimefanyika katika maeneo makuu mawili ya jiji hilo,Soko Kuu na Stendi Kuu.

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania aliyepaswa kuwa mgeni rasmi,Rombo aliwapongeza wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi hilo la usafi lililoanza mapema saa 12 asubuhi.

“Mazingira lazima yawe safi kwa ajili ya afya zetu. Na ili yawe safi, ni jukumu letu sisi wananchi kuyatunza kwa kufanya usafi mara kwa mara,” alisisitiza Rombo.

Aidha, alihoji tabia ya baadhi ya wananchi kutojitokeza kushiriki katika shughuli hizo muhimu na kutaka sheria ndogo ndogo za jiji zianze kutumika ipasavyo kuratibu zoezi la usafi katika maeneo yote ya mkoa wa Arusha.

Kwa upande wao, wananchi walioshiriki waliunga mkono hatua hiyo ya kuhamasisha usafi, wakieleza kuwa maeneo kama masoko na stendi ni nyenzo kuu za kupata kipato, hivyo yanahitaji kuwa safi kila wakati ili biashara ziendelee kufanyika kwa ufanisi.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yamebeba kaulimbiu ya kimataifa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa vizazi vijavyo. Maadhimisho hayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika tarehe 5 Juni 2025 katika Jiji la Dodoma, ambapo Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.