SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka waandishi wa habari kuendelea kutoa habari zinazohusu miendendo ya viongozi wa umma hasa wale wanaokiuka maadili ya utumishi bila woga.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Saalaam na Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi, wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari. Alisema vyombo vya habari vinaweza kutumia njia mbalimbali kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu hali ya uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi wa umma nchini.
Alitaja baadhi ya njia hizo kuwa ni vikaragosi, picha jongefu, tahariri, makala na kwamba habari hizo zinasaidia sana kuwafanya viongozi kuzingatia matakwa ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
“Zipo taarifa nyingi tunazozifanyia kazi ambazo bila jitihada zenu, tusingezijua kwasababu vyombo vya habari vimekuwa mdau na msaada wetu mkubwa katika kukusanya taarifa muhimu na za ukweli zinazoipa nguvu jamii kujua hali ya uadilifu nchini,” alisema.
Alisema lengo la kukutana na wahariri ni kuelimishana na kubadilishana mawazo kuhusu uadilifu wa viongozi wa umma nchini. Jaji mstaafu alisema lengo la sekretarieti hiyo ni kuendeleza ushirikiano mwema kati ya sekretarieti na vyombo vya habari kupitia kwa wahariri na waandishi wa habari.
Alisema sekretarieti imekuwa ikipokea taarifa kutoka vyanzo mbali mbali kuhusu mwenendo wa watumishi wa umma na kuzichakata kabla ya kuzitangaza kwa umma. Alitaja majukumu ya sekretarieti hiyo kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, kupokea matamko ya raslimali, maslahi namadeni na kuyafanyia uchunguzi.
Jaji mstaafu alitaja jukumu lingine kuwa ni kufanya uhakiki, kufanya utafiti wa hali ya uadilifu nchini, kutoa ushauri katika mambo ya uadilifu na kubuni mikakati ya ukuzaji wa maadili nchini. “Tunafanya hivi kuwajengea weledi wa kutosha ili mnaposikia jambo muwe na ufahamu wa kutosha kabla ya kulitangaza. Hatua hii itasaidia kuongeza weledi na ulinganifu utakaozingatia uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia Ibara ya 18 ya Katibaya mwaka 1977, Sheria ya Maadili yay a viongozi wa Umma, Kanuni zake na misingi ya taaluma yenu ya habari,” alisema .
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED