Katibu wa AMCOSS Maswa afungwa jela kwa rushwa, uhujumu uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:20 PM May 25 2025
Katibu wa AMCOSS Maswa afungwa jela kwa rushwa, uhujumu uchumi
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Katibu wa AMCOSS Maswa afungwa jela kwa rushwa, uhujumu uchumi

Mahakama ya Wilaya Maswa imetoa hukumu kwa Masanja Andrew Mboje (36) ambaye ni Katibu wa AMCOS ya Gula, kifungo cha miaka 20 jela na kutakiwa kurejesha fedha kiasi cha Tsh 3,518,000/= alizofanyia ubadhirifu.

Katibu huyo alishtakiwa kwa makosa ya Ubadhirifu na Ufujaji kinyume na Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022] Mei 20 mwaka huu. Ikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022].

Ilidaiwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa akiwa Katibu wa AMCOS ya Gula na mtu pekee aliyekasimiwa mamlaka ya kununua pamba kutoka kwa wakulima, alitumia kwa matumizi yake binafsi fedha kiasi cha Shilingi 3,518,000/= alizopaswa kumlipa mkulima wa pamba Bw. Edward James Mathias.

Shauri hilo la Uhujumu Uchumi namba 196/2025 limesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa Azizi Mzee Khamis (RM) na Wakili wa Serikali Bahati Madoshi Kulwa.