Tanzania, Cuba zasaini mkataba kuhamisha teknolojia, utengenezaji viuatilifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:49 PM May 04 2025
news
NDC
Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Dk. Nicolaus Shombe akibadilishana mkataba na Mkurugenzi wa Kampuni ya Labiofam, Julio Gonzallez wa Cuba.

TANZANIA na Cuba zimesaini mkataba wa kuhamisha teknolojia ya utengenzaji wa Viuatilifu Hai (Biolarvicides) kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa malaria na wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, Tanzania imeweka lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria katika Bara la Afrika, huku ikilenga kutokomeza ugonjwa huo barani kote ifikapo mawaka 2030. 

Mkataba huo umesainiwa baina ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), kupitia Kampuni tanzu ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) yenye shughuli zake Kibaha mkaoni Pwani, pamoja na serikali ya Cuba kupitia Kampuni ya Labiofam, leo jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk. Nicolaus Shombe, amesema uhaulishaji wa teknolojia hiyo, kutoka kwa wataalamu wa Cuba, unatoa haki miliki (patent right) ya asilimia 100 kwa Tanzania, ambapo itaifanya nchi kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa za viuatilifu hai duniani. 

Amesema mbali na Cuba, Tanzania itakuwa mzalishaji tegemezi wa dawa za magonjwa yatokanayo na mbu pamoja na bidhaa za viuatilifu hai, ikijumuisha viuatilifu vya mimea (Bio-pesticides) uzalishaji wa mbolea hai (Bio-fertilizers) na virutubisho vya chakula, hali itakayo saidia kuinua sekta ya kilimo kwa nguvu nchini. 

“Baada ya makabidhiano ya teknolojia hii, uzalishaji wa bidhaa zote za viuatilifu zitakuwa chini ya hati miliki ya NDC kupitia kampuni ya TBPL. Ambapo itahakikisha upatikanaji wa bidhaa za kilimo hususani viuatilifu na dawa za malaria.” 

Ameendelea kusema: “Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, bidhaa zitakazozalishwa zitalinda mazingira ya Tanzania kwa kuwa hazitakuwa na sumu. Pia itasaidia kuzalisha dawa za malaria na kusaidia kuondoa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.” amesema Shombe. 

Aidha, akizungumza baada ya utiaji saini, Mkurugenzi wa Kampuni ya Labiofam, Julio Gonzallez, amesema uhaulishaji wa teknolojia hiyo ni matokeo ya uhusiano mzuri uliopo kati ya serikali ya Tanzania na nchi ya Cuba. 

Amesema toka mwaka 2017 uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zilizotokana na teknolojia hiyo, ulikuwa chini ya serikali ya Cuba, hivyo kufikia hatua ya utiwaji saini ya kuhamisha hati miliki, unaenda kuipa fursa Tanzania, kumiliki kiwanda cha pili kwa ukubwa duniani katika uzalishaji bidhaa za viuatilifu. 

“Hakuna shaka ya uhusiano kati ya Tanzania na Cuba, teknolojia hiyo itaisaidia Tanzania kujua namna bidhaa zinavyotengenezwa na kuendelea kuzalisha dawa zote.” amesema Gonzallez.