WAFUASI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria akiwemo Katibu wa Kanda hiyo, Zakaria Obadi wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiingia katika kanisa Katoliki la Kirumba lililopo Ilemela, Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CHADEMA imeeleza kuwa viongozi wao pamoja na Wanachama wamekamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Kirumba, Ilemela, Mwanza. Taarifa hiyo imeeleza kuwa wafuasi hao wamekamatwa wakiwa wanaingia Kanisani Kirumba kusali na kuwaombea wathirika wote wa vitendo vya utekaji ndani na nje ya chama hicho.
Kwa mujibu wa baadhi ya wafuasi wa Chama hicho, siku ya leo ilipangwa rasmi kwa ajili ya kuwaombea wathirika hao waliowataja kama mashujaa kupitia ibada ya Jumapili. "Kila aliyekuwa amevalia Sare ya Chama au ana viashiria vya kuwa Mwanachama wa CHADEMA amekamatwa na mpaka muda huu wamekamatwa viongozi na wanachama 25. Tuko katika harakati za kuwadhamini," ameeleza mmoja wa wafuasi hao.
Akiongea na Nipashe digital leo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Gidion Msuya amethibitisha kukamatwa kwa wafuasi.Kuhusu tuhuma zinazowakabili Msuya, amesema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi na kuwa baadaye litatoa taarifa kamili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED