RC Mhita: Wafanyabiashara wekeni vitambuzi vya moto kuepuka hasara

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 04:29 PM Oct 26 2025
 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na wananchi pamoja baadhi ya wafanyabiashara waliopata athari ya moto iliyotokea jana katika mtaa wa Igalilimi kata ya Kahama mjini.
PICHA: SHABAN NJIA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na wananchi pamoja baadhi ya wafanyabiashara waliopata athari ya moto iliyotokea jana katika mtaa wa Igalilimi kata ya Kahama mjini.

MKUU wa mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaweka vitambuzi vya moto katika maeneo yao ya biashara, ikiwa ni hatua ya kujikinga na majanga ya moto yanayoweza kusababisha hasara kubwa za mali.

Mhita ameyabainisha haya leo wakati wa ukaguzi wa athari zinazotokana na janga la moto iliyotokea jana usiku majira ya saa tatu katika mtaa wa Igalilimi kata ya Kahama mjini na kati ya maduka 13 maduka sita yameungua na saba yameokolewa.

 Amesema, kumekuwa na matukio kadhaa ya moto katika masoko na majengo ya biashara na yanayotokana na uzembe na ukosefu wa vifaa vya tahadhari na kuwataka kila mfanyabiashara kuweka vifaa hivyo ili kujikinga na athari za moto zinazosababisha biashara kuungua na kudidimia kiuchumi.

 “Tuwe na utamaduni wa kujikinga kabla ya majanga kutokea. Wafanyabiashara wote wahakikishe majengo yao yana vifaa vya kutambua moto mapema pamoja na vizima moto. Hii itasaidia kupunguza hasara na kulinda maisha ya wananchi wetu”Amesema Mhita.

1

 Aidha Mhita amesema, wengi waliweka vifaa hivyo hawapati majanga ya namna hiyo na kuwataka mamlaka husika kuendelea kutoa elimu juu ya majanga ya moto na yanadhibitika kwa urahisi tofauti na majanga meingine ambayo yamekuwa yakitokea mara kadhaa.

 Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, ASF, Fatma Sato walipopata taarifa walifika kwa wakati na kuzima moto kwa kushirikiana na wananchi pamoja na mgodi wa barrick Buzwagi na hakuna majeruhi wala vifo.

 Amesema, Moto ulikuwa mkubwa kutokana na baadhi ya maduka ya biashara kuwa na magodoro, vitambaa, nguo pamoja na maboksi na chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika moja ya duka.

 Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga, SCAP Janeth Magomi nae amesema, baada ya kupata taarifa hizo walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuhakikisha wanalinda mali za wamiliki wa maduka ili zisiweze kuibiwa na wananchi na wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa mpaka moto ulipozimwa.