Gonga FC, Rorya Utd mwisho wa ubishi nusu fainali Umoja Cup leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:24 PM Oct 26 2025

Kikosi cha cha Mabingwa Watetezi wa Umoja Cup Rorya, Gonga Fc
Picha: Mpigapicha Wetu
Kikosi cha cha Mabingwa Watetezi wa Umoja Cup Rorya, Gonga Fc

MTIFUANO mkali wa michuano ya Umoja Cup Rorya 2025, unatarajiwa kushuhudiwa leo, Jumatatu katika mechi ya nusu fainali kati ya Mabingwa Watetezi, Gonga FC na Rorya United.

Katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Maji Sota, Rorya, mashabiki wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushudia timu ya kwanza itakayokata tiketi ya kutinga fainali.

Hiyo ni baada kushuhudiwa upinzani mkali katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, kwa timu tatu kufuzu nusu fainali kupitia mikwaju ya penalti.

Katika michuano hiyo, ambayo imeingia hatua ya nusu fainali, Gonga FC ndiyo timu pekee iliyovuka kwa ushindi wa ndani ya dakika 90 huku zingine tatu zikifuzu kwa mikwaju ya penalti.

Gonga ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, waliitupa nje Kabwana FC kwa kuichapa bao 1-0, shukrani kwa bao la Nyawaya Juma dakika ya  79.

Mabingwa watetezi hao, watashuhudiwa tena leo wakishuka katika Uwanja wa Maji Sota kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza dhidi ya Rorya United iliyofuzu hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Samary FC baada ya sare ya mabao 2-2.

Kuelekea mechi hiyo ya nusu fainali ya kwanza, Afisa Habari wa Rorya United, David Owino, chini ya kaulimbiu yao ya 'Hii ni Yetu', amesema, "tunaamini kesho (leo), ndio utakuwa mwisho kwa Gonga FC kutamba."

Alisema kikosi chao kinejiandaa vizuri kuweza kuibuka na ushindi na kwenda fainali kulibeba taji hilo mwaka huu.

Nusu fainali ya pili itapigwa kesho katika uwanja huo, ambapo timu mbili zilizotinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti; Masonga FC na Bubombi FC zitamenyana.

Bubombi ilifuzu hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya KMT FC  baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1. 

Kwa upande wa Masonga FC yenyewe ilitinga nusu fainali ya Umoja Cup Rorya 2025 kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Bukura FC baada ya sare ya mabao 2-2.

Akizungumzia michuano hiyo, Mwenyekiti wa Mashindano hayo, Ochieng Meli, alisema maandalizi yote ya hatua ya nusu fainali yamekamilika na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange huo.

Alisema baada ya nusu fainali hizo mbili leo na kesho, ratiba hiyo itasimama keshokutwa kupisha uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kabla ya kuendelea tena Alhamisi Oktoba 30, mwaka huu, kwa mchezo wa fainali.

Kwa upande wa Afisa Habari wa Umoja Cup, Nasibu Francis, aliziomba klabu zilizotinga hatua ya nusu fainali kufanya maandalizi mazuri kuelekea michezo yao ijayo ili kuepukana na lawama baada ya kupoteza michezo yao.

"Tumeona hatua ya nane bora timu nyingi zimekuwa na maandalizi yasiyo mazuri, hivyo kupoteza michezo yao na lawama nyingi wakizipeleka kwa waamuzi wa michezo husika, pasipo kuangalia kuwa maandalizi yao kuanzia vikosi vyao vilikuwa hafifu mno," alisema Francis huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani.
 
Naye Katibu wa Umoja Cup, Telly Miki, alisema, "katika hatua ya robo fainali tumeona timu bora na zenye maandalizi bora zaidi zikifanya vema na kupata matokeo na kuendelea na mashindano.

"Katika hatua hii ya nusu fainali tunategemea kupata burudani safi na yenye ushindani mkubwa zaidi kwani timu zipo tayari na zimejipanga vema kwa mashindano haya."

Michuano hiyo ya kila mwaka, hudhaminiwa na mdau mkubwa na mpenda soka wilayani Rorya, Peter Owino, ikiwa na lengo la kudumisha amani, ushirikiano, umoja, kutoa burudani na kuibua vipaji.