SMAUJATA yawataka wananchi kupaza sauti kupinga ukatili

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 03:06 PM Dec 28 2025
Katibu wa SMAUJATA Hasna Maige
PICHA: MARCO MADUHU
Katibu wa SMAUJATA Hasna Maige

JUMUIYA ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilaya ya Shinyanga imewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili katika jamii, huku ikisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwa vyombo husika ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Wito huo umetolewa jana wakati wa uzinduzi wa kikundi cha kusaidiana kwenye shida na raha kiitwacho Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, chenye makao makuu yake Ihapa, Kata ya Oldshinyanga. Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu wa SMAUJATA wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni mlezi wa kikundi hicho, Hasna Maige, amesema wananchi wanapaswa kupinga vitendo vya kikatili kwa kutolea pia taarifa matukio hayo, ili kudumisha amani ndani ya jamii.

1

Amesema katika kikundi hicho, hatarajii kusikia wanachama wa wakijihusisha na vitendo vya ukatili, bali wanapaswa kuwa mabalozi wa kupinga vitendo hivyo na kuhakikisha jamii inakuwa salama. “Naiomba sana jamii isifumbie macho vitendo vya ukatili, ukiona mtu au mtoto anafanyiwa vitendo hivyo, zuia na toa taarifa kwenye vyombo husika, ili hatua za haraka zichukuliwe kabla ya kutokea madhara,” amesema Maige.

Aidha, amewataka wanachama hao kuishi kwa upendo, mshikamano na amani, pamoja na kuepuka kuingiza masuala ya itikadi za kisiasa ndani ya kikundi. Mwenyekiti wa Kikundi hicho Juma Bugohe, amesema wanajumla ya wanachama 83, na kuwataka wanachama washirikiane pamoja na kufuata miongozo na katiba ya kikundi.
2

Nao baadhi ya wanachama wamesema wameamua kujiunga na kikundi hicho kwa lengo la kusaidiana katika shida na raha, wakisisitiza kuwa umoja ni nguvu na chachu ya maendeleo. Katika uzinduzi huo, wanachama wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng’ombe walijadili rasimu ya katiba yao, ikiwa ni sehemu ya kuweka misingi ya uendeshaji na mustakabali wa kikundi hicho.
Mwisho.