Diwani wa Puni awasihi bodaboda wasitumike kuivuruga amani ya nchi

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 04:17 PM Dec 14 2025
Diwani wa Puni wilayani Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu akitoa elimu kwa vijana wa bodaboda, Njiapanda ya Didia wilayani humo, wasitumike kuivuruga amani ya Tanzania
PICHA: MARCO MADUHU
Diwani wa Puni wilayani Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu akitoa elimu kwa vijana wa bodaboda, Njiapanda ya Didia wilayani humo, wasitumike kuivuruga amani ya Tanzania

DIWANI wa Kata ya Puni, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu, amewapongeza vijana wa bodaboda wa eneo la Njiapanda ya Didia kwa kuendelea kudumisha amani, na kuwasihi wasitumike vibaya kuivuruga amani na watu wachache wasioitakia mema Tanzania.

Rajabu ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na vijana hao, akiwahimiza kuilinda amani ya nchi kwani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi. Amesema endapo amani ya nchi itavurugika, shughuli za maendeleo zitasimama, hali itakayowaathiri zaidi vijana wanaojitegemea kwa kufanya kazi za kila siku, ikiwamo waendesha bodaboda.

 “Amani ya nchi ikivurugika, shughuli za maendeleo zitasimama na ninyi mtashindwa kujipatia kipato cha kuendesha maisha yenu na kuhudumia familia zenu, kwa sababu mtajikuta mkiwa ndani ya ‘lockdown’,” amesema Mhandisi Rajabu.

“Nawashukuru sana vijana wa bodaboda kwa kuendelea kudumisha amani na kukataa kutumika kufanya maandamano yasiyo na afya. Amani ni tunu ya Taifa letu, hivyo tuilinde kwa wivu mkubwa na tumtetee Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, mama mwenye huruma na mwenye uchu na maendeleo ya wananchi,” amesema Mhandisi Rajabu.

 Kwa upande wao, vijana wa bodaboda wakiongozwa na Paul Laurent wamesema hawapo tayari kutumika kuvuruga amani ya nchi, wakieleza kuwa wao ndiyo waathirika wakubwa pindi vurugu zinapotokea, kwani hushindwa kufanya shughuli za kujipatia kipato na familia zao kukosa mahitaji ya msingi.

 Wamesema matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, na siku ya Uhuru, Desemba 9, kuambiwa  kubaki majumbani, yamewaathiri pakubwa kutokana na maisha yao kutegemea kutoka nje kufanya kazi ili kupata ridhiki.

 James Lugembe, ameiomba serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kudumisha amani ya nchi, ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi bila hofu.