Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewasimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TEMESA pamoja na kurugenzi yake kufuatia uchunguzi uliofichua ubadhirifu wa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 ndani ya taasisi hiyo.
Hatua hiyo imefuata ripoti ya tume maalumu iliyoundwa ndani ya miezi miwili kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma. Akitangaza uamuzi huo, Waziri Ulega alisema serikali haitavumilia vitendo vinavyoathiri uadilifu wa taasisi za umma, huku akisisitiza kuwa wote waliohusika katika upotevu wa fedha hizo watafikishwa katika vyombo vya sheria. Aidha, ameagiza tume ndogo kukamilisha majibu kuhusu wahusika wote ndani ya siku saba ili hatua za ziada zichukuliwe mara moja.
Ameyazungumza hayo wakati wa ziara ya Mradi wa Maendeleo ya Kivuko cha Nyunya–Nyamisati na kutoa maagizo kwa wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi. Alisema mradi huo ni muhimu kwa wakazi wa Mafia ambao wanategemea kivuko hicho kwa usafiri na shughuli zao za kila siku.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.4 unahusisha Kampuni ya Korea kwa ushirikiano na kampuni ya mzawa ya DMG. Hadi sasa, mkandarasi ameshapokea malipo ya awali ya shilingi bilioni 4.3 na anatakiwa kuharakisha utekelezaji ili kuendana na matarajio ya serikali.
Waziri Ulega alisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo, hivyo hakuna nafasi kwa uzembe au ucheleweshaji usio na sababu. Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kukamilisha miradi ya miundombinu kwa wakati ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema pia kuwa ni muhimu vijana wa maeneo yanayozunguka mradi kushirikishwa katika shughuli za ujenzi ili kunufaika na ajira zitokanazo na uwekezaji wa serikali. Kwa mujibu wake, miradi ya kimkakati lazima iwaletee wananchi fursa na kuboresha maisha yao.
Katika hotuba yake, Waziri Ulega alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani akibainisha kuwa amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aliwaonya vikali wakandarasi na watumishi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya ubadhilifu kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali bila upendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigamboni, Haran Sanga, amepongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Ujenzi na kuiomba serikali kuendelea kufanya maboresho katika vivuko vingine nchini. Amesema kuwa uwepo wa vivuko imara ni muhimu kwa kuwawezesha wananchi kuvuka kwa urahisi na kuchochea shughuli za kiuchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED