WATU watano wamekamtwa kwa tuhuma za ulanguzi wa tiketi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Magufuli jijini Dar es Salaam.
Walikamatwa juzi baada ya kufanyika ukaguzi wa kushtukiza wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini(LATRA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi. Baadhi ya walanguzi hao, walikamatwa wakiwa na tiketi za karatasi mkononi ambazo waliwauzia kwa gharama kubwa wasafiri wanaokwenda katika mikoa mbalimbali kupitia kituo hicho cha Magufuli.
Akizungumza baada ya kukamatwa watuhumiwa hao, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, amesema anataka wachukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo kama hivyo.
Kadhalika, Suluo amesema katika kukomesha vitendo hivyo, wanaboresha kanuni na taratibu za usafirshaji, ili watu wote wanaofanya kazi za uwakala wa abiria kwenye mabasi wasajiliwe na watambulike kisheria.

“Tutataka ukiwa wakala, utuambie ni wa gari gani na watakuwa na vitambulisho maalum na watapewa kibali na LATRA cha uwakala wa basi, huwezi kuwa wakala halafu unaumiza watu, na kwa namna hii tutawabana,”alisema Suluo.
Suluo amesema mamlaka hiyo itaendelea kuboresha sekta hiyo ili kuhakikisha usafiri wa ardhini unakuwa ni staha na salama kwa kila anayeutumia. Pia, amesema katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, wanaendelea kufanya ukagudhi wa mara kwa mara.
Tayari mamlaka hiyo, imeshatoa vibali 72 vya muda mfupi kwa ajili ya watoa huduma ya usafirishaji kuongeza magari katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambacho kinakuwa na abiria wengi wanaosafiri kwenda mapumziko kwenye mikoa mbalimbali nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED